Serena afichua siri kujitoa Rogers Cup

Muktasari:

Nyota huyo mwenye miaka 36, ni bingwa wa mataji 23 ya Grand Slam kwa wanawake kwa wachezaji mmoja mmoja, alisema aliamua kujitoa baada ya shutuma kuhusu mwanae kuzidi.

Los Angeles, Marekani. Mcheza tenisi nyota wa Marekani, Serena Williams, amefichua kilichosababisha ajitoe kwenye michuano ya Rogers Cup inayoendelea nchini Canada.
Nyota huyo mwenye miaka 36, ni bingwa wa mataji 23 ya Grand Slam kwa wanawake kwa wachezaji mmoja mmoja, alisema aliamua kujitoa baada ya shutuma kuhusu mwanae kuzidi.
Alisema baada ya kushutumiwa sana na ndugu na jamaa zake alikaa na kutafakari kisha akabaini kuna ukweli kwamba yeye yu mkosaji kwa kumuacha mwanae wa miezi 11 na kwenda kushiriki mashindano ya tenisi.
“Mwanangu alizaliwa Septemba 2017, mimi tangu Julai nilishaanza kumuacha kwa saa nyingi nikijiandaa kwa mashindano ya Wimbledon badaye nimekuja huku kweli najiona mkosaji kwa mwanangu,” alisema.
Serena alichapwa kwa seti mbili za 6-1, 6-0 na Mwingereza Johanna Konta katika mashindano ya Silicon Valley Classic, ikiwa mara ya kwanza kwake kushindwa katika raundi ya awali ya michuano yoyote ile tangu mwaka 1995 alipoanza kucheza tenisi ya kulipwa.
Siku mbili baadaye ndipo akatangaza kujitoa kwenye Rogers Cup, jana aliandika kwenye mtandao wake wa  Instagram kwamba anajiona mkosaji kwa kutoyapa kipaumbele malezi ya binti yake.
“Kwa kweli ninajichukia mwenyewe na kujiona mimi sio mama mwema kwa mwanangu, lakini nimeshwaeleza mama ya dada yangu kuhusu hili, baada ya kubaini kosa langu nimejirudi sasa nataka kutoa nafasi ya kipekee kwa malezi ya mwanagu,” aliandika katika akaunti yake.