Sarah Ramadhan hataki habari hizo kabisa

USICHEKE! Lakini huo ndio ukweli, kwa wale wanariadha waliozoea kudanganya kwa kukubali kupandishwa bodaboda ili wamalize mbio wa kwanza ni maadui namba moja kwa Sarah Ramadhan.

Hiyo ya kupanda bodaboda au kupita shotikati unaambiwa sio ishu tena kwenye mbio ndefu zinazofanyika nchini, kwani katika mbio 10 lazima tatu ziwe na watu wa aina hiyo ambao wanatumia udanganyifu ili kupata fedha za zawadi.

“Ni bora nikimbie kwa kufuata njia halali hata nikimaliza wa mwisho kuliko kudanganya, ukijizoea hivyo utabaki kukimbia hapa hapa nchini,” anasema Sarah.

Mwanariadha huyo aliyetwaa medali ya fedha kwenye mbio za Mbeya Tulia Marathoni hivi karibuni anasema mtindo wa kukatisha ruti au kupanda bodaboda kwa mwanariadha ili amalize mbio wa kwanza unafanyika sana tu hapa Bongo.

“Ukizoea hivyo, Ulaya huwezi kukimbia maana kule hudanganyi, bora ukomae tu kihalali hadi umalize kuliko kudanganya,” alisema.