Sanga aenguliwa, Kidau freshi TFF

Clement Sanga

Muktasari:

  • Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema jana kuwa, uamuzi huo ulitokana na kikao cha kamati yao ya utendaji ambayo pia imeridhia ongezeko la idadi ya wachezaji 10 wa kigeni kutoka saba wa awali na wote wakiruhusiwa kucheza mchezo mmoja.

KAIMU Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ameenguliwa katika nafasi yake ya Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, huku Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likimtangaza rasmi Wilfred Kidau kuwa Katibu Mkuu.

Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema jana kuwa, uamuzi huo ulitokana na kikao cha kamati yao ya utendaji ambayo pia imeridhia ongezeko la idadi ya wachezaji 10 wa kigeni kutoka saba wa awali na wote wakiruhusiwa kucheza mchezo mmoja.

Karia alisema kwanza kamati yao imekubaliana kumsimamisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Clement Sanga kwa kukosa sifa stahili.

“Yanga walileta barua ya kukataa kwa Mwenyekiti wao si Sanga bali ni Yusuf Manji hivyo kupoteza sifa kuu ya kuwa katika nafasi hiyo na tutaanza mchakato wa kusaka mwenyekiti mpya wa nafasi hiyo,” alisema Karia.

Pia alisema kamati imeridhia na kupitisha Kidau kuwa Katibu Mkuu baada ya kuikaimu kwa muda mrefu.

Karia alisema wataboresha ratiba ya Kombe la FA kutoka timu 80 hadi 100 ama zaidi, huku timu za Ligi Kuu lazima ziwe na timu za vijana U17-20 ambazo zitacheza ligi zao kadhalika wataboresha Ligi daraja la kwanza na Ligi daraja la pili.

NYOTA WA KIGENI

Karia pia alisema TFF imekubali kuziongezea klabu idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 10 wanaoweza kutumika wote katika mechi moja.

“Tutaweka kanuni ngumu kwa timu kutaka kumsajili mchezaji yoyote wa kigeni ili kupata waliokuwa bora na wanastahili katika Ligi yetu tupo katika hatua za mwisho kuzipitia sheria hizo na tutaziweka wazi siku si nyingi, “ alisema Karia.

“Wachezaji ambao wapo sasa katoka klabu za Ligi Kuu na hawana vigezo hivyo hatutawatoa ila walimaliza mikataba yao tunataka wasajiliwe waliokuwa na vigezo stahili na tutasimama na ukali katika hili,” alieleza Karia na kuongezea hayo yalikuwa ni makubaliano na klabu za Ligi Kuu Bara.

Naye Kidau alisema walichokubaliana mpaka kuongeza wachezaji ni kuwepo ushindani katika Ligi Kuu.

Kidau alisema kuvutia wadhamini wengi kujitokeza kudhamini ligi na hata timu shiriki na wachezaji wazawa kupata ushindani wa kutosha kutoka kwa wageni.

“Hii ni fursa wachezaji wa wazawa nao kuanza kufikiria zaidi kucheza soka la nje, na timu ya Taifa ikiitwa kuwe na wachezaji wengi kutoka nje ya Tanzania, msimu uliopita ulikuwa na nyota wa kigeni 40 katika timu 16 sawa na asilimia nane ndio maana tumekubaliana na klabu kuongezea idadi, “ alisema Kidau.