Samuel Eto’o atua Qatar

London, England. Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona, Inter Milan na Chelsea, Samuel Eto’o, anakamilisha taratibu za kujiunga katika Ligi Kuu ya Qatar kukipiga katika klabu ya Qatar Sports Club ya Ligi Kuu.

Klabu hiyo ya Qatar ilitangaza jana kuwa mshambuliaji huyo aliyekuwa tegemeo kwenye timu ya Taifa ya Cameroon kabla ya kustaafu soka la kimataifa mwaka juzi, anasajiliwa akiwa mchezaji huru.

Eto’o mwenye miaka 37, baada ya kuondoka Chelsea, alisajiliwa na timu za Antalyaspor na Konyaspor za Uturuki.

Mshambuliaji huyo alitarajiwa kukamilisha taratibu zote na kutambulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Eto’o ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Cameroon, mataji mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika na mchezaji bora mara nne wa tuzo ya mwanasoka bora baranini Afrika na mshindi wa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ujio wake unatarajiwa kuitangaza kwa kiasi kikubwa timu ya Qatar Football Club na Ligi ya Qatar kwa ujumla wake.

Awali mshambuliaji huyo aliahidi kwenda kumalizia soka lake nchini Ufaransa lakini ameghairi na kuamua kumalizia nchini Qatar, nchi itakayoandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022.