Samatta amtaka Ulaya dogo wa Serengeti Boys

Muktasari:

Chipukizi Kelvin John alionyesha kiwango cha juu katika mashindano ya kufuzu kwa Afcon kwa vijana

Dar es Salaam.Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga klabu ya Genk kule Ubelgiji, amemtabiria makubwa nyota wa Serengeti Boys, Kelvin John kuwa atafika mbali zaidi yake.

Samatta alisema anatamani kumuona Kelvin akifikia mafanikio makubwa zaidi kwenye soka kwani, ana kiwango na uwezo mkubwa dimbani.

Pia, alimchana straika huyo kinda kuwa mafanikio aliyonayo kwa sasa hayajapatikana kwa urahisi hivyo, akamtaka kuwa na nidhamu na kufanya mazoezi kwa nguvu.

"Wapo vijana wengi wanatamani kufika hapa nilipo, lakini wanapaswa kuwekeza akili na jitihada kwenye kile wanachotaka kuwa nacho. Kwangu nimepambana sana, haya mafanikio hayajapatikana kwa urahisi kabisa, nimetoka mbali sana.

"Ana uwezo ila akitaka kufanikiwa na hata kunizidi ni lazima aongeze juhudi, nimezungumza naye na kumpa nasaha zangu,” alisema Samatta.

"Tanzania kuna vipaji vikubwa sana na katika michuano ya kufuzu AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, niliviona vipaji vingi ambavyo vinavyotakiwa kuendelezwa," alisema.