Salamba, MO wana tiketi ya Simba

SIMBA imepania kutwaa ubingwa wa michuano ya SportPesa Super Cup leo Jumapili na mastaa wake wawili wapya, Adam Salamba na Mohammed Rashi wamepewa kazi maalumu.

Nyota hao wawili waliojiunga na Simba hivi karibuni, wanatarajiwa kuongoza mashambulizi wakati timu hiyo ikiikabili Gor Mahia leo Jumapili.

Simba ilifuzu hatua ya fainali kwa kuiondosha Karibagi Sharks na Kakamega Homeboys wakati Gor Mahia wao walizifunga JKU mabao 3-0 na Singida United 2-0.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wamekuwa na wakati mgumu wa kufunga bao katika mechi mbili zilizopita lakini kaimu kocha mkuu, Masoud Djuma ana matumaini mastaa hao watashangaza wengi.

Simba inaendelea kuwakosa mastaa wake wawili, John Bocco na Emmanuel Okwi waliofunga mabao 34 Ligi Kuu msimu uliopita. Kukosekana kwao kunatoa nafasi kwa Salamba aliyefunga mabao manane msimu huo pamoja na Rashid aliyeifungia Prisons ya Mbeya mabao 10.

Djuma alisema hawezi kuweka wazi namna ambavyo atakipanga kikosi chake, lakini kwenye mazoezi ya mwisho alionekana kuwatumia zaidi nyota hao.

“Tunaiheshimu Gor Mahia, ni timu nzuri na kubwa lakini tutacheza vizuri. Mechi hii ya fainali tunatarajia kuonyesha uwezo wa juu zaidi ya michezo mingine yote tuliyocheza mpaka sasa,” alisema kocha huyo wa zamani wa Rayon Sport ya Rwanda.

Naye nahodha wa Simba mjini hapa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema wanataria kupata ushindi mkubwa kutoka kwa mabingwa hao wa Kenya lakini lengo lao ni kuondoka na ubingwa.

Mara baada ya mchezo huo wa fainali, Simba itapaa kurudi nchini na moja kwa moja kuingia kambini, Sea Scape, jijini Dar es Salaam kabla ya kesho asubuhi nyota wa timu hiyo kwenda kupimiwa suti na viatu.

Suti na viatu hivyo wanavyonunuliwa na Mo Dewji ni maalum kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya utoaji wa tuzo za klabu hiyo zinazotolewa usiku wa kesho Jumatatu, jijini Dar es Salaam.