Salamba, MO Rashid kuipeleka Simba England

Muktasari:

  • Nyota hao wawili waliojiunga na Simba hivi karibuni, wanatarajiwa kuongoza mashambulizi wakati timu hiyo ikiikabili Gor Mahia leo Jumapili.

Nakuru. Simba imepania kutwaa ubingwa wa mashindano ya SportPesa Super Cup leo Jumapili basi mastaa wake wawili wapya, Adam Salamba na Mohammed Rashid wamepewa kazi maalum.

Nyota hao wawili waliojiunga na Simba hivi karibuni, wanatarajiwa kuongoza mashambulizi wakati timu hiyo ikiikabili Gor Mahia leo Jumapili.

Simba ilifuzu hatua ya fainali kwa kuiondosha Karibagi Sharks na Kakamega Homeboys wakati Gor Mahia wao walizifunga JKU mabao 3-0 na Singida United 2-0.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wamekuwa na wakati mgumu wa kufunga bao katika mechi mbili zilizopita, lakini kaimu kocha mkuu, Masoud Djuma ana matumaini makubwa kuwa huenda mastaa hao wakawashangaza wengi.

Simba inaendelea kuwakosa mastaa wake wawili, John Bocco na Emmanuel Okwi waliofunga mabao 34 Ligi Kuu msimu uliopita.

Kukosekana kwao kunatoa nafasi kwa Salamba aliyefunga mabao manane msimu huo pamoja na Rashid aliyeifungia Prisons ya Mbeya mabao 10.

Djuma alisema hawezi kuweka wazi namna ambavyo atakipanga kikosi chake hii leo lakini kwenye mazoezi ya mwisho alionekana kuwatumia zaidi nyota hao.

“Tunakwenda kucheza fainali ngumu na ya aina yake. Siwezi kusema kama nitawapanga wachezaji fulani na wengine watakaa benchi, ila tutacheza vizuri,” alisema Djuma.

“Tunaiheshimu Gor Mahia, ni timu nzuri na kubwa lakini tutacheza vizuri. Mechi hii ya fainali tunatarajia kuonyesha uwezo wa juu zaidi ya michezo mingine yote tuliyocheza mpaka sasa,” alisema kocha huyo wa zamani wa Rayon Sport ya Rwanda.

Akizungumzia kitendo cha kuachiwa mikoba hiyo na aliyekuwa bosi wake, Pierre Lechantre aliyetimuliwa, Djuma alisema amewahi kuongoza timu kwenye fainali kadhaa hivyo haitakuwa kitu kigeni kwake.

“Nimeongoza timu kwenye fainali nyingi,  hii itauwa mwendelezo tu wa pale nilipoishia. Mimi siyo mgeni hapa Simba, nimeshasimamia timu kwa wakati fulani na nitaendelea kufanya hivyo kweye fainali,” alisema.

Naye nahodha wa Simba mjini hapa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema wanataria kupata ushindi mkubwa kutoka kwa mabingwa hao wa Kenya lakini lengo lao ni kuondoka na ubingwa.

“Haijalihi kama Gor Mahia wamefunga mabao mangapi na sisi tmefunga mangapi kwenye mechi zilizopita. Hii ni fainali, atakayecheza vizuri ndiye atakuwa bingwa,” alisema beki huyo wa kushoto.

“Wachezaji wote wako kwenye ari nzuri na wamejipanga ili kuweza kushinda mchezo huu wa mwisho. Tunafahamu kwamba mashabiki wengi wanatufuatilia,” aliongeza

 

GOR MAHIA WANENA

Wakati huo huo, Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr alisema amezungumza na wachezaji wake juu ya umuhimu wa mechi hiyo hivyo hatma yote ipo kwao kuipa ubingwa timu hiyo ama la.

Kerr alisema pamoja na kwamba walifanya vizuri kwenye mechi zilizopita ikiwemo mchezo mgumu dhidi ya Singida United, wanahitaji kutulia ili kushinda fainali hiyo.

Kocha huyo aliyefundisha zaidi soka kwenye nchi za Vietnam na Afrika Kusini, alisisitiza kuwa kutokana na uimara wa Simba kwenye mikwaju ya penalti, wangependa kumalizika mchezo huo ndani ya dakika 90.

“Simba wana hali ya kujiamini linapokuja suala la penalti. Wamefanya vizuri kwenye penalti zilizopita hivyo watakuwa kwenye nafasi kubwa ya kufanya vizuri. Kikubwa kwetu ni kumaliza mchezo mapema, ndani ya dakika 90,” alisema Kerr.

“Haijalishi kwamba nimewahi kuifundisha Simba ama la, ila kikubwa ni wachezaji kupambana. Tunataka kwenda kucheza tena na Everton, tena awamu hii ni kwao,” alisisitiza.

Naye nahodha wa Gor Mahia, Haruna Shakava alisema watapambana na kucheza soka safi ili kushinda mchezo huo wa aina yake.