Salah, Morata lao mmoja

Friday January 12 2018

 

LIVERPOOL, ENGLAND

HII kitu usiwaambie kabisa mashabiki wa Liverpool hawawezi kukuelewa. Kwamba eti, inasemakana lakini Mohamed Salah ndiye mchezaji aliyepoteza nafasi nyingi za wazi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Salah huyu huyu. Huyu huyu unayemfahamu, mwenye mabao 17 kwenye Ligi Kuu England hadi sasa na anayevutia kumtazama mpira unapokuwa kwenye miguu yake huku akifukuzia kimyakimya Kiatu cha Dhahabu.

Lakini, kwa data zilizokusanywa na Arseblog, zinaonyesha kwamba Salah anaongoza kwa kupoteza nafasi za wazi zilizokaribia kuwa mabao baada ya kufanya hivyo mara 15 na kufuatiwa na straika wa Chelsea, Alvaro Morata, aliyekosa nafasi 14.

Mastaa wawili wa Manchester City, Sergio Aguero na Gabriel Jesus wanashika nafasi ya tatu na nne kwa kukosa nafasi 12 na 11 mtawalia, huku Christian Benteke wa Crystal Palace akikamilisha tano bora kwa kukosa nafasi 11.

Kwa namna ambavyo Salah amekuwa akitupia msimu huu ni jambo gumu kukubali kwamba anaongoza kwenye kupoteza nafasi, lakini ukweli unabaki palepale kuwa kama angetumia vizuri nafasi zote alizopata, basi kwa sasa angekuwa ameshatupia mabao 30 huko.

Lakini, Liverpool hawajali hilo, ilimradi kwa sasa anawafanya kuwa tishio ndani ya uwanja. Shughuli anayo Morata, The Blues hawamwelewi kabisa. Straika huyo Mhispaniola aliboronga tena kwenye mechi dhidi ya Arsenal usiku wa juzi Jumatano, huku akiwa amefunga mabao 12 tu katika mechi 26 alizochezea Chelsea. Morata pia amefulia mbaya baada ya kufunga mara tatu tu katika mechi zaidi ya 13 alizocheza mara ya mwisho.