Salah, Misri wasubiri muujiza Saudi Arabia

Muktasari:

Russia imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia

Moscow, Russia. Matumaini ya Mohamed Salah na Misri kubaki katika Kombe la Dunia ni kuomba Saudi Arabia iifunge Uruguay kesho baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa wenyeji Russia.

Wenyeji Russia wakiwa katika kiwango bora zaidi iliwalazimu kusubili hadi kipindi cha pili kupata ushindi huo muhimu na uliowaweka vizuri katika Kundi A.

Russia ilipata bao la kwanza baada ya kujifunga kwa beki wa Misri, Ahmed Fathi akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Aleksandar Golovin katika dakika 47.

Kuingia kwa bao hilo kuliwapoteza Misri na kujikuta wakiruhusu mabao mawili ya haraka dakika 59 na 62.

Dakika ya 59, Mshambuliaji wa Russia Denis Cheryshev alifunga bao lake la tatu katika Kombe la Dunia na kumfikia Cristiano Roanldo katika orodha ya vinara wa ufungaji.

 Wakati Misri wakijiuliza nini kinatokea Russia ilipata bao la tatu lililofungwa na Artem Dzyuba kwa shuti kali lililompita topo kipa wa Misri, Elshenawy katika dakika 62.

Matokeo hayo yameiweka Russia katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa mara yakwanza kwa hatua ya 16 bora wakiwa na rekodi ya kufunga mabao nane.

Salah alifunga bao lake la kwanza katika Kombe la Dunia katika dakika73 kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa na kwenye eneo la hatari.

Penalti hiyo ya Misri ilibidi kutumika kwa teknolojia VAR kuthibisha ndipo mwamuzi akakubali ipigwe na Salah hakufanya makosa.

Matokeo hayo yanaifanya Misri kuendeleza rekodi yake mbaya katika Kombe la Dunia pamoja na kusubili kwa miaka 28 kufuzu kwa fainali hizo.

Vikosi

Russia: Akinfeev, Fernandes, Kutepov, Ignashevich, Zhirkov, Zobnin, Gazinsky, Samedov, Golovin, Cheryshev, Dzyuba.

Akiba: Lunev, Semenov, Kuzyaev, Dzagoev, Smolov, Kudryashov, Granat, Aleksey Miranchuk, Anton Miranchuk, Erokhin, Smolnikov, Gabulov.

Misri: El Shenawy, Fathi, Gabr, Hegazi, Abdel-Shafy, Hamed, Elneny, Salah, Said, Trezeguet, Mohsen.

Akiba: El Hadary, Elmohamady, Gaber, Morsy, Kahraba, Ashraf, Sobhi, Hamdy, Shikabala, Samir, Warda, Ekramy.

Mwamuzi: Enrique Caceres (Paraguay)