Safari ya Chirwa Simba bado ipo

Obrey Chirwa

Muktasari:

Msimu huu Simba ambayo inanolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre imefanya usajili wa maana na wa pesa nyingi kuliko timu zingine za ligi kuu.

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu Bara ndio zimepamba moto na vinara wa ligi hiyo, Simba wameahidi msimu huu ni lazima kitaeleweka tu.

Msimu huu Simba ambayo inanolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre imefanya usajili wa maana na wa pesa nyingi kuliko timu zingine za ligi kuu.

Yaani hata mahasimu wao, Yanga wanasubiri mbele ya pesa iliyotumika kusajili ndani ya Simba.

Lakini, achana na usajili huo ambao matunda yake yataonekana siku chache zijazo kama watabeba ndoo ama la, ishu kubwa ni mbio za usajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Kwa sasa Simba ina huduma ya mastraika wawili matata sana, nahodha John Bocco na Emmanuel Okwi ambao kwa pamoja wamepasia nyavuni mara 28.

Hata hivyo, Simba imepanga kufanya usajili wa maana mwishoni mwa msimu huu ili kutengeneza kikosi cha kutisha kwenye soka barani Afrika, kwa kusajili mastaa wakubwa wa ndani na nje ya nchi.

Sasa Mwanaspoti linakuletea mastaa watano ambao wanaweza kutua ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa na kulingana na mahitaji waliyonayo kwa sasa.

Obrey Chirwa

Ukitaka kuwatoa roho mashabiki wa Yanga basi mzungumzie vibaya straika wao, Mzambia Obrey Chirwa. Ndio mshambuliaji tegemeo kwenye kikosi cha George Lwandamina, lakini mara kadhaa amekuwa akihusishwa kwenda Simba.

Ndio, Mwanaspoti linafahamu tayari mabosi wa Simba wameanza mikakati ya kunasa saini ya Chirwa, ambaye mkataba wake na mabingwa hao watetezi unafikia tamati Julai, mwaka huu. Mpaka sasa hajasaini mkataba mpya na Yanga hivyo, kuzidisha tetesi yuko njiani kwenda Simba na kinachosubiriwa kwa sasa ni kumalizika kwa ligi tu ili amalizane na mabosi wa Simba.

Chirwa ameshafunga magoli 12 katika ligi mpaka sasa na Simba inamwona kama mtu sahihi wa kusimama mbele ya lango la wapinzani pindi anapokosekana Bocco au Okwi.

Pia, straika huyo anaweza kucheza pacha na Okwi ama Bocco kutokana na kuwa na uzoefu mkubwa kwenye ligi na mechi za kimataifa. Chirwa anajua kufungana ana mguvu na mbinu za kukabiliana na walinzi wakorofi kama Kelvin Yondani, Yakub Mohammed na wengine. Kama Chirwa atasaini Simba basi anaweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kutengeneza pacha matata.

Habibu Kyombo

Mabeki wa Yanga na timu zingine za Ligi Kuu Bara wanaijua shughuli yake. Kyombo, mshambuliaji hatari wa Mbao FC amepachika mabao tisa mpaka sasa na kama atacheza na viungo wanaojua kupiga pasi za mwisho kama Haruna Niyonzima, Mkude, Mzamiru ama Ndemla basi hiyo Simba weka mbali na watoto.

Kyombo anaweza kuwa straika chaguo la pili nyuma ya Bocco, Okwi ama Chirwa kwa wakati mmoja na kama akiwa anaingia kama sub anaweza kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.

Mbao wamefunga magoli 21, katika mechi 22, ambazo wamecheza katika ligi kwa hesabu rahisi tu kuwa Kyombo amefunga nusu ya magoli ya timu hiyo na kama atakuwa ndani ya kikosi cha Simba, anaweza kufunga zaidi.

Eliud Ambakile

Mshambuliaji wa Mbeya City amefunga magoli tisa na naiona nafasi yake katika kikosi cha Simba kama watamkosa Kyombo ambaye ameshaanza kunyemelewa na Yanga na Azam ambao nao wanahaha kuimarisha safu zao za ushambuliaji.

Mbeya City wamefunga magoli 20, katika mechi 22 za Ligi Kuu Bara ambazo wamecheza mpaka sasa lakini Ambokile licha ya kucheza katika timu iliyo kwenye wakati mgumu kiuchumi ameweza kufunga nusu ya magoli ya timu nzima.

Ni wazi mshambuliaji wa aina hii anaonekana ni mkali na anauwezo wa kucheza katika timu kubwa kama Simba ambayo ni lazima kujiimarisha katika safu yao ya ushambuliaji ambayo akikosekana Bocco na Okwi huwa katika mazingira magumu.

Ambokile kama akijituma na kuweza kufanya ambacho anafanya msimu huu akiwa na Mbeya City anaweza kuwa lulu katika kikosi cha Simba kwa aina yake ya uchezaji na kutamani kufunga muda wote lakini ikiwa vingine na hivyo anaweza kushindwa kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Peter Mwalyanzi aliyesajiliwa na Simba kutoka timu hiyo.

Benedict Tinoco

Kipa namba moja kwa sasa katika kikosi cha Mtibwa Sugar ameweza kuwa imara zaidi na kuimalika mara baada ya kuanza kupata nafasi ya kucheza msimu huu baada ya Said Mohammed ‘Nduda’ ambaye alikuwa kipa namba moja kwenye kikosi hiko kujiunga na Simba.

Tinoco ameweza kuwa katika kiwango imara, lakini naiona nafasi yake katika kikosi cha Simba kwa sababu kipa namba moja Aishi Manula amecheza kwa muda mrefu na mfululizo na ameanza kuwa na majeraha ya hapa na pale na kukosa baadhi ya mechi kama ilivyokuwa Taifa Stars dhidi ya Algeria na aliumia na kutaka kutoka katika mechi dhidi ya Njombe Mji lakini alipata matibabu na akamaliza mechi kwa maumivu.

Nduda ambaye ni kipa namba mbili nae amekuwa maji kupwa maji kujaa kwa kusumbuliwa na maumivu ya goti na si wa kumtegemea wakati wote kwani muda wowote anaweza kupata majeruhi na akashindwa kuwepo golini.

Emmanuel Mseja ambaye ndio kipa namba tatu ameshindwa kuaminiwa kwa kuwa ameshindwa kuwa na matokeo mazuri kwani katika kombe la Mapinduzi amecheza mechi nne na kufungwa magoli manne.

Naiona nafasi ya Tinoco kwani anauzoefu kwa kuwa alishacheza katika timu ya Yanga akiwa kama akipa namba tatu na kama atakuwepo katika kikosi cha Simba anaweza kuongeza nguvu na kushindana na Manula pamoja na Nduda.

Himid Mao

Nahodha wa Azam Himid Mao mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu na kama watashindwa kumpa mkataba mpya kama walivyoshindwa kufanya kwa Bocco, Manula, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe naiona nafasi yake ndani ya kikosi cha Simba.

Simba inaviungo wakabaji wawili ambao ni James Kotei na Jonas Mkude, ambao wamekuwa wakicheza vizuri lakini Mwanaspoti ilizungumza na kocha wa Simba Pierre Lechantre kudai kuwa kipindi cha usajili ataongeza mchezaji mmoja katika eneo hilo.

Himid ambaye ndio kiungo bora mkabaji kwa sasa hapa nchini kwa kuwa anapata nafasi ya kucheza na kuanza katika kikosi cha Taifa Stars ni rafiki wa karibu wa Kapombe na Bocco kama Azam watashindwa kumpa mkataba mpya sitashangaa kusikia amesaini mkataba msimbazi.

Yote kwa yote Himid anauwezo wa kucheza katika kikisi cha kwanza katika timu yoyote hapa nchini na kama Simba watafanikiwa kumpata kutokana pia na ukaribu wao na Azam kikosi chao kitaimarika zaidi ya kilivyokuwa msimu huu.