Saa 120 kuipeleka Stars Afcon

Muktasari:

  • Tanzania mara ya mwisho kufuzu kwa Afcon ilikuwa 1980 nchini Nigeria

Dar es Salaam. Hesabu nzuri katika mechi mbili dhidi ya Cape Verde zitakazochezwa ndani ya muda wa siku tano, zitaiweka timu ya Taifa, ‘Taifa Stars' kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) mwakani nchini Cameroon.

Ushindi wa mechi mbili ngumu dhidi ya Cape Verde, ugenini na nyumbani ndani ya muda usiozidi saa 120, utaifanya Taifa Stars kuhitaji pointi moja tu itakapovaana na Uganda na Lesotho ili kufuzu fainali hizo.

Taifa Stars inayosaka nafasi ya kushiriki Afcon kwa mara ya kwanza tangu ilipofuzu mwaka 1980, ikiibuka na ushindi kwenye mechi ya kwanza ugenini itakayochezwa Oktoba 12 na marudiano Oktoba 16, itafikisha pointi nane ambazo zitaiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu sanjari na timu nyingine moja kwenye ya Kundi L kati ya Cape Verde, Uganda au Lesotho.

Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda uliopo baina ya mechi ya kwanza na pili, benchi la ufundi chini ya Kocha Emmanuel Amunike, linapaswa kuandaa mbinu na mipango bora ya kiufundi ili kuiwezesha timu hiyo isiathirike na ratiba ya kucheza mechi mbili ndani ya siku chache kuvuna pointi sita muhimu.

Nje ya Uwanja, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeanza kuchukua hatua za kuhakikisha ufinyu huo wa ratiba ya mechi mbili mfululizo dhidi ya Cape Verde haiathiri programu ya timu.

Mkakati wa kwanza katika maandalizi ya timu hiyo ni kukodi ndege maalumu itakayoipeleka timu nchini humo na kuirudisha nyumbani haraka nchini kujiandaa na mechi ya marudiano.

“Kwa kuwa tunaanzia kwao, Cape Verde wametupa taarifa rasmi mchezo utachezwa Oktoba 12 na mchezo wa marudiano na sisi tumepanga utachezwa Oktoba 16.

“Kutokana na ukaribu wa mchezo TFF na Kampuni ya Bia ya Serengeti tunatazama namna ya kupata usafiri ambao utatufanya baada ya mchezo wa kwanza turudi tuwahi mechi ya marudiano," alisema Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.

TFF inaonekana kujifunza kutokana na makosa yaliyotokea kwenye harakati ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2015, ambapo ufinyu wa ratiba ulisababisha Taifa Stars kuondolewa kwa aibu mbele ya Algeria kwenye raundi ya pili.

Mechi hizo mbili ambazo Taifa Stars ilicheza nyumbani na ugenini ndani ya muda wa siku nne kuanzia Novemba 14 hadi 17, ilitolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 9-2. Timu hiyo ilitoka sare ya mabao 2-2 jijini kabla ya kuchapwa 7-0 nchini Algeria.