Rwambiti, Limuru Starlets hapatoshi fainali Wanyama

Muktasari:

Balozi wa michuano hiyo inayoshirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 15-20, ni Kiungo wa Tottenham Hotspurs na nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama.

Nairobi. KITENDAWILI cha nani ataungana na Limuru Starlets kwenye fainali ya kusaka bingwa wa kanda ya kati, katika  michuano ya Chapa Dimba, kimeteguliwa baada ya Rwambita Girls kujikatia tiketi.

Rwambiti Girls kutoka kaunti ya Kirinyaga iliiondosha Express Queens kutoka Laikipia kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 kumalizika timu zote zikitoshana nguvu kwa kufungana 1-1.

Katika mchezo huo wa Nusu fainali ya pili uliokuwa na ushindani mkubwa, ni Express ndio iliyotangulia kupata bao kunako dakika ya 20, kupitia kwa Muregoro Mary aliyeingia kuchukua nafasi ya Naserian Agness.

Hata hivyo, wakati Express wakishangilia ushindi walijikuta wakipoteza muelekeo na kuruhusu Rwambiti kusawazisha bao kupitia kwa Njeri Juliet Wakari (23).

Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika lakini milango yote ilikuwa migumu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi hiyo hiyo lakini hadi Mwamuzi wa mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Chuo cha Ufundi cha Thika, John Ndung'u anapuliza kipyenga bado matokeo yalikuwa 1-1.

Ili kumpata mbabe, ikabidi hatua ya matuta ihusike ambapo kipa wa Rwambiti, Jane Muthoni aliibuka shuja kwa kupangua mikwaju mitatu ya penalti na kuihakikishia klabu yake ushindi wa 3-2 (4-3).

Wafungaji wa penalti kwa upande wa Rwambiti walikuwa ni Bancy Waruri, Mercy Wairimu na Selina Wangechi huku Nangala Mildred na Moureen Muthoni wakiifungia Express.

Kwa matokeo hayo, Rwambiti itamenyana na Limuru Starlets kesho ambapo mshindi atapata nafasi ya kushiriki fainali za kitaifa zitakazofanyika Machi 24, kwenye dimba la Bukhungu, mjini Kakamega pamoja na kushindia kitita cha Ksh. 200,000.