Ruaha Marathon yaja na mipango mizito

Muktasari:

  • Akizungumza na wanahabari, Mratibu wa mashindano hayo, Frank Mwaisumbe alisema kuwa  lengo  la mashindano hayo ni kuhamasisha utalii Nyanda za Juu Kusini, Utunzaji wa Mazingira hasa mto Ruaha na kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya michezo

Iringa. MASHINDANO ya  Mbio za Ruaha Marathon yanatarajia kunguruma tena mkoani Iringa Julai 21 baada ya kutofanyika kwa miaka kadhaa tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza na wanahabari, Mratibu wa mashindano hayo, Frank Mwaisumbe alisema kuwa  lengo  la mashindano hayo ni kuhamasisha utalii Nyanda za Juu Kusini, Utunzaji wa Mazingira hasa mto Ruaha na kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya michezo

Mwaisumbe alisema kuwa lengo jingine la mashindano hayo ya riadha ni kuibua vipaji vya wanaridha katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwani tangu mwaka 2011 Ruaha Marathoni  imeibua vipaji vya vijana ambao wengi wao wanashiriki mbio za kitaifa na kimataifa.

Aliongeza kuwa licha ya kuibua vipaji vya vijana mashindano hayo sehemu ya kutambua na vipaji kwa ajili ya vijana na kutengeneza mazingira ya ajira kwa wale ambao wanataka kufanya mbio hizo kuwa ajira watapelekwa katika vyuo vinavyofundisha jinsi ya kukimbia kwa utaalamu ili waweze kufikia malengo yao.

Mwaisumbe alisema kuwa mwaka 2011 mbio hizo zilianza kufanyika hadi 2014 na zilisimama baada ya kuwa na mambo mengi lakini  kwa sasa zimeanza tena mbio za tano julai 21 mwaka huu ambazo zitakuwa na mbio fupi za kilometa tano, kilomita 21 na ndefu za kilimita 42.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela amewataka wadau na watanzania wengi kushiriki mbio hizo kwa lengo la kushiriki maendeleo ya mkoa huo kwa sababu kitakachopatikana asilimia 35 ya fedha zitaenda kujenga kituo cha Afya.

Alisema kuwa zinahitajika zaidi ya Milioni 700 kwa ajili ya kuboresha kituo cha afya cha Ngome kwa kuwa sasa kimezidiwa na wagonjwa na hivyo wengi wao kuhamishiwa hospitali ya manispaa ya Frelimo au mkoa.

Alisema kuwa mashindano hayo kwa sasa yanakabiliwa changamoto ya wadhamini, na kuwaomba  wadau wajitokeze na sio kwa kukimbia pekee hata kwa michango kwani kutokana na mashindano hayo wadau wanachangia ujenzi wa kituo hicho.