Ronaldo amfunga mdomo Salah

Muktasari:

Ronaldo ni mwanasoka bora wa mwaka wa dunia, wakat Salah ni mwanasoka bora wa Afrika

Nyon, Uswisi. Mshambuliaji Cristiano Ronaldo amemthibitishia Mohamed  Salah  kuwa yeye ni mwanasoka bora wa dunia baada ya kuiongoza Ureno kuichapa Misri 2-1 jana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Mshambuliaji  wa Liverpool, Mo Salah alifunga bao la kuongoza kwa Misri dakika 55, lakini Ronaldo alijibu mapigo kwa kufunga mabao mawili katika dakika mbili 92 na 95 katika ushindi huo wa Ureno.

Salah aliingia katika mchezo huo akiwa na rekodi ya kufunga mabao manne wakati Liverpool ikichakaza Watford, alithibisha kasi yake ya kuzifumania nyavu kwa kufunga bao la kuongoza kwa Misri likiwa ni goli lake la 37 msimu huu katika mashindano yote.

Nyota wa Real Madrid, Ronaldo akiwa katika ubora wake waliwanyamazisha mashabiki wa Misri kwa kufunga bao la kusawazisha dakika 92, lakini kabla hawajakaa sawa akapachika bao la pili dakika 95 na kumfanya kufikisha magoli 23 katika michezo 14 aliyocheza.

Timu hizo zimekutana mara nne, Ureno imeshinda mechi tatu na Misri ikishinda mechi moja hivyo wanaingia uwanjani wakitaka kuweka rekodi hiyo sawa.

Misri kwa sasa ipo nafasi ya 44 kwenye viwango vya ubora wa Fifa wakati Ureno mabingwa wa Ulaya wakiwa nafasi ya tatu katika viwango hivyo.