Ronaldo ameshinda mtihani wa mashabiki

Muktasari:

  • Matokeo ya mechi hiyo, yalikuwa ni sare ya mabao 3-3 ambapo staa huyo Ronaldo aliweza kuipa timu yake pointi moja na pia kuweka rekodi ambayo iliwafurahisha mashabiki wake na kuwanyima raha wafuasi wa Lionel Messi.
  • Wakati Ronaldo akiacha kicheko kwa wafuasi wake, ikawa ndivyo sivyo kwa staa wa Argentina Lionel Messi ambaye alikosa penalti dhidi ya Iceland na kuwafanya mashabiki wake wanyimwe raha na kukosa la kutamba nalo mtaani.

Dar es Salaam. NI Cristiano Ronaldo pekee mshambuliaji wa Real Madrid, ndiye alitimiza ndoto za mashabiki wake, kwenye Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao matatu dhidi ya Hispania, akiwa na timu yake ya Ureno, katika mechi ya kwanza.
Matokeo ya mechi hiyo, yalikuwa ni sare ya mabao 3-3 ambapo staa huyo Ronaldo aliweza kuipa timu yake pointi moja na pia kuweka rekodi ambayo iliwafurahisha mashabiki wake na kuwanyima raha wafuasi wa Lionel Messi.
Wakati Ronaldo akiacha kicheko kwa wafuasi wake, ikawa ndivyo sivyo kwa staa wa Argentina Lionel Messi ambaye alikosa penalti dhidi ya Iceland na kuwafanya mashabiki wake wanyimwe raha na kukosa la kutamba nalo mtaani.
Ronaldo na Messi ni wapinzani wakali ni kama Simba na Yanga hapa Tanzania ambapo hawawezi kuungana na kuwa kitu kimoja kushirikiana katika mambo ya kuendesha soka, bali kila mmoja anakuwa anapenda mwenzake aharibikiwe.
Kitendo cha Messi kuipa timu yake pointi moja na kutoka kapa kwenye mechi ya kwanza, kimempa kichwa Ronaldo kuendelea kuonekana yeye mbabe kwenye ulimwengu wa soka hasa Kombe la Dunia.
Lakini bado mashabiki wa Messi wanaendelea kuvuta subra wakisubilia huenda akafanya kitu cha tofauti katika mechi zinazoendelea.
Supastaa mwingine wa  Brazil,  Neymar Jr naye alitarajia na wengi kufanya maajabu kama waliyozoea wakimuona akifanya kwenye ligi za Ulaya, lakini wakabakia na maumivu ya moyo baada ya kushindwa kufunga dhidi ya  Uswisi ambayo walitoka nayo kwa sare ya bao 1-1.
Mwanaspoti Online limefanya mahojiano na mastaa mbalimbali wa ligi ili kuchangia changamoto ambayo wanakutana nayo mastaa hao na kufanya tofauti na matarajio yao.
Pato Ngonyani ni staa wa Yanga, alisema Messi na Neymar Jr walishindwa kufungwa kwa sababu ya presha kutoka timu pinzani ambao walikuwa wanapaki basi.
"Wale ni mastaa wa Dunia, wanachokifanya katika ligi zao kinaonekana na ndicho kinachowafanya wawe na upinzani mkali, mfano mzuri Messi alikuwa anakabwa na mabeki zaidi ya watatu,"anasema.
Naye staa wa Azam FC, Joseph Kimwaga anasema Neymar Jr alishindwa kufunga kutokana na sababu mbili ambazo ni kukabwa na mbwembwe ambazo ziliwafanya wapinzani wake watumie kama silaha.
"Wakati Neymar anataka kuonyesha ufundi wake, upinzani ulikuwa umemkamia kiasi kwamba akajikuta ni mtu anayechezewa rafu wakati wowote,"anasema.