Ronaldo aanza kutupia mabao Juventus

Muktasari:

  • Juventus ilikuwa ikicheza na kikosi chao cha vijana chini ya miaka 20 na kuifunga kwa mabao 5-0, mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Agnelli, ulio kwenye viwanja vya Villar Perosa.

Milan, Italia. Mshambuliaji mahiri wa Ureno, Cristiano Ronaldo jana alifungua akaunti yake ya mabao kwenye timu yake mpya ya Juventus, baada ya kufunga bao murua katika mchezo wake wa kwanza.

Juventus ilikuwa ikicheza na kikosi chao cha vijana chini ya miaka 20 na kuifunga kwa mabao 5-0, mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Agnelli, ulio kwenye viwanja vya Villar Perosa.

Ronaldo, mwenye miaka 33 aliyejiunga na Juve akitokea Real Madrid mwezi uliopita licha ya kuanza mazoezi tangu Julai 30 hakupata kucheza mchezo wowote wa kirafiki kati ya ile ambayo timu hiyo ilicheza ikiwa ziarani Marekani.

Katika mchezo huo Ronaldo alianza kwa kufunga bao la kwanza katika dakika ya nane akiupeleka mpira juu ya kipa Leonardo Loria, kabla ya kashikashi zake kumfanya Riccardo Capellini dakika 10 baadaye.

Mchezaji Paulo Dybala aliifungia timu hiyo bao la tatu na la nne dakika ya 31 na 40 na Claudio Marchisio akahitimisha ushindi kwa bao la dakika ya 53.

Hata hivyo mchezo huo ilibidi uvunjike kabla ya wakati kutokana na msshabiki karibu 5,000 waliohudhuria kuvamia uwanja wakishangilia na kutaka kusaliamiana na wachezaji katika dakika ya 72.

Mshambuliaji Leonardo Bonucci, aliyerejea Juve wiki mbili zilizopita baada ya kuichezea AC Milan msimu uliopita, Emre Can, aliyetokea Liverpool, walianza huku mkongwe Mario Mandzukic, Sami Khedira na Miralem Pjanic wakianzia benchi.

Ronaldo anatarajiwa kuanza kuitumikia Juventus katika Ligi Kuu ya Italia Jumamosi ijayo katika mchezo dhidi ya Chievo Verona.

Mshambuliaji huyo baadaye aliandika katika akaunti yake ya Twitter, akiwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa sapoti wanayompa.