Ronaldo: Nitapambana na Messi mpaka kieleweke!

Muktasari:

Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amefikisha tuzo tano sawa na mpinzani wake Lionel Messi.

PARIS, UFARANSA. Cristiano Ronaldo amesema ataendeleza ‘vita’ na mpinzani wake mkubwa Lionel Messi katika mbio za kuwania tuzo za mchezaji bora wa dunia.

Ronaldo alitoa kauli hiyo muda mfupi, baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora akimshinda Messi. Mshambuliaji huyo wa Real Madrid imefikisha tuzo tano sawa na mpinzani wake.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG) Neymar. Tuzo hizo zinatolewa Ufaransa na kura zinapigwa na waandishi wa habari 173.

“Nitapambana naye (Messi), nitahakikisha nakuwa kwenye kiwango bora. Nitacheza vizuri kwa klabu na timu ya taifa,” alisema Ronaldo alipoulizwa kuhusu nafasi ya Messi.

Alisema ataendelea kulinda kipaji chake kwa manufaa ya Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno kwa kucheza kwa kiwango bora.

“ Nina furaha. Hili ni tukio kubwa katika maisha yangu, napenda kutoa shukurani kwa wachezaji wenzangu wa Real Madrid, pia nawashukuru watu wote walionifikisha hapa,” alisema Ronaldo.

Wakati wa kutoa shukurani, Ronaldo alitania anataka kupata watoto saba. Nguli huyo ana watoto wanne aliozaa na wanawake watatu tofauti. Nyota huyo alikwenda Paris na ndege binafsi akiongozana na familia yake.