Riadha Polisi yapania mashindano ya EAPCCO

Muktasari:

  • Timu hiyo ina jumla ya wanariadha 15 katika mbio za kati pamoja na mbio ndefu za uwanjani huku wanariadha wa mbio fupi wakipiga kambi jijini Dar es Salaam wakijifua chini ya kocha mwingine.

Arusha. Kocha Mkuu wa timu ya Riadha ya Polisi Tanzania, Rogath Stephen ambao wamepiga kambi mkoani hapa kwa zaidi ya miezi mitano kujiandaa na mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Polisi (EAPCCO), wamehaidi kunyakua medali za kutosha.
Timu hiyo ina jumla ya wanariadha 15 katika mbio za kati pamoja na mbio ndefu za uwanjani huku wanariadha wa mbio fupi wakipiga kambi jijini Dar es Salaam wakijifua chini ya kocha mwingine.
“Mchezo wa Riadha ni kutengeneza muda bora sio kumaliza nafasi ya kwanza na kwa muda wanaoutumia sahivi wakati wa mazoezi ni mzuri na hii ni faida ya kuweka kambi Arusha sehemu yenye baridi hivyo watakapofika eneo la mashindano wanakuwa na kazi nyepesi”alisema Rogath.
Hata hivyo upungufu wa wanariadha jinsia ya kike imekuwa changamoto kwani katika kikosi cha wanariadha 15 alionao wanawake wapo watatu pekee Jenifa Saning’o anayeshiriki mita 100, Mariam Mohamedi wa mita 800, 1,500 na 3,000 pamoja na Fabiola Willium 5,000 mita na 10,000 mita.
Upungufu huo unamuweka katika mazingira magumu jinsi ya kuunda timu ya kupokezana vijiti (Relay) kwa maana wanahitajika wanariadha wanne katika mchezo huo.
Timu hiyo inaotarajia kuondoka Agosti mbili kwenda kuungana na wenzao katika mashindano hayo yanayotarajia kuanza kufanyika Agosti sita huku baadhi ya michezo itakayokuwepo ni pamoja na soka, taekwondo, sarakasi, ngumi, kulenga shabaha, netiboli, na kikapu.
Kwa mara ya kwanza mashindano hayo yalifanyika mwaka jana Nchini Uganda na wenyeji kuibuka vinara wa jumla wakifuatwa na Kenya huku Tanzania iliyopeleka wanamichezo 10 kati yao wanariadha sita na Taekwondo wanne na kumaliza nafasi ya tatu.
Alisema Nchi zitakazoshiriki kwenye mashindano hayo yanayoendeshwa kwa mfumo wa Olimpiki ni wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudani, Sudani Kusini, Somalia, Djibouti, Burundi, Rwanda, na Eritrea.