Rest in Peace Ngwea

Muktasari:

  • Ataagwa kesho Jumapili katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika kijiji anachoishi mama yake mzazi, Kihonda mkoani Morogoro. Ni umbali wa kilomita 210 kutoka Dar es Salaam.

ALIONDOKA akiwa anatembea kwa miguu yake, lakini leo Jumamosi saa nane mchana wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wataupokea mwili wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukiwa umelala ndani ya jeneza, amefariki na ndio muda wake wa kuishi duniani umemalizika. Ni Albert Mangwea ‘Ngwea’ mwanamuziki aliyejijengea jina kwenye Bongo flava.

Wanaojua muziki iwe mashabiki, wadau au hata wasanii wenzake wa Bongo, wanakiri ni mkali wa ‘free style’ (mtindo huru) kwani hakuwa na mpinzani.

Kifo chake kimegubikwa na maswali mengi yenye utata kuliko majibu. Mwili wake unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo Jumamosi saa nane mchana ukitokea Johannesburg, Afrika Kusini  alikofikwa na mauti.

Ataagwa kesho Jumapili katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika kijiji anachoishi mama yake mzazi, Kihonda mkoani Morogoro. Ni umbali wa kilomita 210 kutoka Dar es Salaam.

Umati wa wasanii na mashabiki wa muziki kutoka kila kona ya Tanzania unatarajiwa kuungana na familia yake kumuaga katika msiba ambao kwa takriban wiki nzima umekuwa gumzo, kila mmoja akizungumza lake.

Kwa kifupi Mangwea alifariki Jumanne asubuhi baada ya kuanguka na kuzimia katika nyumba aliyofikia huko Afrika Kusini. Alipopelekwa katika Hospitali ya St. Hellen, hakuamka tena ndipo taarifa za kifo chake zikaanza kusambazwa.

Jumanne, zilisambaa taarifa ambazo zilidai alikunywa pombe kupitiliza. Hata hivyo baadaye ilikuja kugundulika kwamba ni uvumi tu wa mitandaoni na ni taarifa za mwanamuziki mwingine aliyepoteza maisha baada ya kupata kilevi kilichopitiliza.

Ripoti kamili ya daktari haijatoka, na uchunguzi ulianza juzi Alhamisi.

Alienda ‘Sauzi’ kufanya nini?

Ilikuwa ni ziara ya kimuziki, aliondoka na msanii mwingine Mtanzania, M2 the P, ambaye ni mwanamuziki mwenzake wanayeelewana kikazi mpaka kwenye maisha ya kawaida. Mangwea alikuwa pamoja na kijana huyo ambaye jina lake halisi ni Mgaza Pembe. Iko wazi kwamba Mangwea alikuwa katika kuutangaza muziki wa Tanzania nje kupitia matamasha.

Hakuwa akiumwa, ila kuna hitilafu za kiafya zilitokea zikasababisha kifo chake huku mwenzake pia akilazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Aliondoka Tanzania Machi 26 mwaka huu, akiambatana na mwenzake huyo na wakati anakumbwa na kifo chake, alikuwa mbioni kurudi Bongo.

Historia yake

Alizaliwa Novemba 16, 1982 jijini Mbeya. Yeye ni mtoto wa mwisho kuzaliwa kwa baba akiwa mtoto wa 10 na kwa mama akiwa mtoto wa sita.

Ngwea asili yake ni Ruvuma, ni mtu wa kabila la Wangoni. Alipokuwa na umri wa miaka mitano, walihamia Morogoro akasoma Shule ya Msingi Bungo alipofika darasa la tano,  baba yake akapata uhamisho kwenda Dodoma.

Baadaye alisoma Shule ya Sekondari ya Mazengo kabla ya kujiunga na Chuo cha Ufundi Mazengo.

Muziki wake

Hadi anakumbwa na mauti alikuwa anawakilisha Kundi la Chamber Squad lililokuwa na makazi yake East Zoo, Dodoma.

Ngwea alikutana na P Funk Majani, Prodyuza maarufu wa Bongo mwaka 2000 na kuanza kufanya kazi naye.

Albamu yake ya kwanza ilikuwa ni ‘a.k.a Mimi’. Alianza kwa kutoa wimbo wa kwanza uitwao ‘Ghetto Langu,’ wimbo huu ulimpatia umaarufu mkubwa.

Ngwea pia aliwahi kushinda tuzo ya Muziki ya Kilimanjaro ya Mwana Hip Hop Bora mwaka 2005. Ana albamu mbili ‘a.k.a Mimi’ na ‘Nge’ aliyoitoa mwaka 2010. Amewahi kuimba nyimbo zilizotamba kama vile Mikasi, She Got a Gwain na nyingine za Dakika Moja, a.k.a Mimi, Gheto Langu, CNN, Demu Wangu, Nipe Dili, Speed 120.

P Funk: Ngwea ana nyimbo 50 ambazo hazijatoka!

Paul Mathyesse, a.k.a P Funk ambaye ni prodyuza aliyefanya idadi kubwa ya muziki wa Ngwea, ameithibitishia Mwanaspoti kuwa hadi sasa haelewi nini kimetokea lakini anachofahamu ni kuwa Albert Mangwea ni zaidi ya msanii kwake.

“Nilikuwa na Ngwea kwa zaidi ya miaka 13 ninamfahamu vizuri na ninaujua uwezo wake, alikuwa ni zaidi ya rafiki yaani sina neno zuri la kusema kumhusu zaidi ya kumtakia safari njema,” anasema kwa uchungu.

P-Funk ambaye ni Mkurugenzi wa Bongo Records ambayo marehemu alikuwa akifanyia kazi zake hadi anafikwa na umauti, anafafanua kuwa hata albamu zote mbili za Ngwea yeye ndiye amezifanya ukiachilia mbali nyimbo ambazo alikuwa akifanya moja moja ambazo hadi sasa wanazo nyimbo 50 ambazo hawajazitumia.

Maneno ya mwisho aliyoandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter Mei 26:

“Namhitaji Mungu kwa kila dakika, kila saa,” akitumia lugha ya Kiingereza.

Maneno ya mwisho kuzungumza na mama yake:

Ilikuwa ni wiki mbili zilizopita Ngwea aliwasiliana na mama yake na kumtaka aendelee kumuombea au waombeane na kumwahidi angerudi Ijumaa iliyopita na hakuwasiliana naye tena hadi anafikwa na umauti.

Chid Benz

Anaonyesha huzuni na masikitiko yake kwa kusema kuwa familia ya muziki imepata pengo, lakini ya hip hop imepata pengo kwa kuwa alikuwa ni zaidi ya mwanamuziki kutokana na uwezo aliokuwa nao.

“Sina cha kufanya zaidi ya kumwimbia wimbo kwa kuwa mimi na yeye ni wanamuziki tunaliwazana kwa muziki, nimetoa wimbo nimeuita Albert Mangwea na umeshaanza kupigwa tangu siku ya pili ya kifo chake,”anasema Chid Benz.

Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’

Anasema kuwa imemuuma kwa kuwa alikuwa ni miongoni mwa marafiki zake wa karibu japo katika siku za hivi karibuni walitengana kutokana na mihangaiko ya kimaisha.

Anaongeza kuwa kuna kipindi akifumba macho anatamani iwe ni ndoto, lakini akifumbua inabaki kuwa kweli, lakini anajipa moyo kuwa ipo siku watakutana kwa kuwa safari hiyo ni ya wote. Mwana Fa aliwahi kuimba wimbo na Ngwea, wimbo huo unaitwa ‘Nisikilize Mimi’.

Mwasiti Almasi

“Inasikitisha kuona kijana kama Ngwea anafariki tena katika kipindi ambacho muziki wa Bongo flava unapoanza kuzaa matunda,”anasema Mwasiti.