Rekodi za Waethiopia zaibeba Yanga Dar

Dar es Salaam.Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga inajivunia rekodi yake nzuri dhidi ya klabu ya Ethiopita baada ya kupangwa dhidi ya Welayta Dicha katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), jana katika droo iliyofanyika mjini Cairo, Misri ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa kati ya Aprili 6 hadi 8 na marudiano itakuwa Aprili 17 na 18.

Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kuzitoa mara mbili klabu za Ethiopia huku wenyewe itolewa mara mmoja tu katika hatua ya mtoano.

Yanga mbali ya kuzitoa timu hizo za Ethiopia lakini inajivunia rekodi yake ya kufunga mabao mengi wanapocheza na Wahabeshi hao.

Hata hivyo pamoja na Yanga kuzionea timu za Ethiopia bado mabingwa hao Tanzania hawajawahi kushinda Ethiopia wakitoka sare mbili na kufunga moja wanapocheza ugenini.

Yanga ilikutana kwa mara ya kwanza klabu ya Ethiopia mwaka 1969, katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika sasa Ligi ya Mabingwa Yanga ilitoa Saint-George ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 5-0.

 Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia timu hizo zilitoka suluhu na mechi ya marudiano Yanga ilishinda 5-0 na kusonga mbele hadi robo fainali.

Yanga ilikutana kwa mara pili Coffee FC Ethiopia mwaka 1998 na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-8, katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia Coffee FC ililazimisha sare 2-2 katika mchezo wa marudiano Yanga ilishinda 1–6 nyumbani na kufanikiwa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Katika Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-4, ilianzia nyumbani na kulazimishwa sare 4-4 na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Ethiopia wenyeji, Dedebit walichapa Yanga mabao 2-0.

Hatahivyo wapinzani wa Yanga wanaoshika nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu Ethiopia, hawana historia au rekodi ya kutisha kwenye mashindano ya Afrika kulinganisha na Yanga.

Endapo Yanga itafanya maandalizi ya kutosha ina nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo kutokana na uzoefu.

Yanga imewahi kufuzu hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa nyakati tofauti.

Dicha haina rekodi ya kujivunia katika soka la Afrika na hata Ethiopia. Mafanikio pekee kwa timu hiyo ni kuwatoa mabingwa wa zamani wa Afrika, Zamalek ya Misri kwenye raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho mwaka huu.

Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009 iliwahi kutwaa ubingwa Ethiopia ulioiwezesha kushiriki Kombe la Shirikisho tofauti na Yanga ambayo imetwaa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 27 na Kombe la FA mara moja ikiwa imeanzishwa mwaka 1935.

 

Urahisi wa Yanga kufuzu hatua ya makundi utachagizwa kwa kiasi kikubwa na ushindi mzuri itakaopata katika mchezo wa kwanza utakaopigwa nyumbani kabla ya kurudiana siku 10 baadaye nchini Ethiopia.

Hakuna namna ambayo Yanga itajitetea endapo itashindwa kutumia vizuri mechi ya kwanza Dar es Salaam licha ya kuwakosa wachezaji wake muhimu watatu wa kikosi cha kwanza bado ina nyota wenye uwezo wa kuipa matokeo mazuri.

Papy Tshishimbi, Said Juma 'Makapu' na Obrey Chirwa watakosa mchezo mmoja kutokana na kupata kadi mbili za njano, lakini nafasi zao zitajazwa na Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na Rafael Daud.