#WC2018: Rekodi yaibeba England kwa Croatia nusu fainali

Muktasari:

Miamba hiyo ilimenyana jana saa 3:00 usiku na leo utapigwa mchezo mwingine wa nusu fainali ya pili ambao utazikutanisha England dhidi ya Croatia.

Moscow, Russia. Wakati jana usiku ulichezwa mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya Ubelgiji na Ufaransa, Kundi G katika mashindano lilionekana kuwa la kifo.

Miamba hiyo ilimenyana jana saa 3:00 usiku na leo utapigwa mchezo mwingine wa nusu fainali ya pili ambao utazikutanisha England dhidi ya Croatia.

England na Croatia zinakutana kwa mara ya nane huku England ikiwa na rekodi bora ikishinda michezo minne dhidi ya miwili ya wapinzani wao na zimetoka sare mara moja.

Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani kote, wengi wakitaka kuona endapo England kama itaondoka na jinamizi la kufanya vibaya licha ya kuwa na kikosi bora au itarudia historia ya kuwa wasindikizaji wa fainali hizo baada ya kutwaa mara moja mwaka 1966 walipokuwa wenyeji.

Bila kujali matokeo ya mchezo wa nusu fainali ya jana na leo, katika fainali za mwaka huu, timu bora zilizoshiriki zimetoka Kundi G.

Ubelgiji iliongoza kundi hilo baada ya kuvuna pointi tisa ikifuatiwa na England (sita), Tunisia (tatu) na Panama iliyoondoka mikono mitupu.

Kwa upande mwingine Croatia imethibitisha haikubahatisha kufika fainali, baada ya kuongoza Kundi D ikivuna pointi tisa na kuiacha Argentina iliyokuwa ikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa ikishika nafasi ya pili kwa pointi nne, Nigeria tatu na Iceland iliondoka mikono mitupu.

Ufaransa iliyopangwa Kundi C iliongoza kwa pointi saba, Denmark (tano), Peru (tatu) na Australia (moja).