Rekodi 10 za Kombe la Dunia, zinazoweza kuvunjwa Russia

Muktasari:

  • Kuelekea michuano ya Kombe la Dunia, inayotarajiwa kutimua vumbi katika miji mbalimbali nchini Russia, Mwanaspoti inaendelea kukuletea baadhi ya mambo unayotakiwa kuyafahamu. Twen'zetu Kombe la Dunia mwanangu, lakini kwanza, kaa tayari kushuhudia rekodi hizi zikivunjwa.

Moscow, Russia. Didier Deschamps, Lionel Messi, Thomas Muller na Cristiano Ronaldo wanafukuzia rekodi kadhaa za Kombe la Dunia. Amini usiamini, Diego Maradona na Mondragon wanaweza wakapoteza rekodi zao.

Kuelekea michuano ya Kombe la Dunia, inayotarajiwa kutimua vumbi katika miji mbalimbali nchini Russia, Mwanaspoti inaendelea kukuletea baadhi ya mambo unayotakiwa kuyafahamu. Twen'zetu Kombe la Dunia mwanangu, lakini kwanza, kaa tayari kushuhudia rekodi hizi zikivunjwa.

1. MAKOCHA WENYE UMRI MKUBWA ZAIDI

Kama Uruguay na Ureno zitakutana kwenye mechi ya hatua ya 16 bora, hesabu zinaonesha kuwa itakuwa ni sawa na miaka 135 na miezi mitatu ya umri wa Oscar Tabarez na Fernando Santos. Sijui tunaelewana?

Yaani, ukijumlisha umri wa makocha hao wawili, Tabarez na Santos, unapata jumla ya miaka 135 na miezi mitatu. Hii ni rekodi mpya. Endapo timu zao zitakutana, basi wanaume hao wataweka rekodi ya kuwa makocha wenye umri mkubwa zaidi kukutana katika mechi moja.

Kama hilo litatokea, amini kwamba watakuwa wamevunja rekodi ya sasa ya miaka 133 na miezi tisa, iliyowekwa na makocha wawili, Otto Rehhagel wa Ugiriki na mwenzake Lars Lagerback wa Nigeria, timu hizo zilipokutana katika michuao ya Kombe la Dunia, yaliyofanyika nchini Afrika Kusini, mwaka 2010.

2. MCHEZAJI MWENYE UMRI MKUBWA

Kipa wa Egypt, Essam El-Hadary, atakuwa na umri wa miaka 45 na miezi mitano, atakaposimama langoni kuongoza taifa lake kucheza mechi yao ya kwanza kwenye kundi lao, dhidi ya Uruguay.

Umri huo unamaanisha kuwa, Nahodha huyo, ataivunjilia mbali rekodi ya Kipa wa Colombia, Faryd Mondragon ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza kwenye Kombe la Dunia. Mwaka 2014, Mondragon, alikuwa na miaka 43 na siku tatu, alipoweka rekodi hiyo.

3. MECHI 13 ZA KOMBE LA DUNIA BILA KUPOTEZA

Rekodi hii inashikiliwa na mabingwa wa kihistoria wa kombe hili, Brazil. Rekodi hii imedumu kwa miongo mingi sana. Baada ya kuchezea kichapo cha 4-2 kutoka kwa Hungary (1954), Brazil walishuka dimbani

katika mechi 13 za Kombe la Dunia bila kupoteza.

Samba Boyz walikuja kufungwa na Hungary haohao, katika michuano ya mwaka 1966. Kuanzia hapo hakuna timu iliyocheza mechi nyingi bila kupoteza.

 

Ujerumani wanakaribia kuvunja rekodi hii, kwani Mara ya mwisho kufungwa ilikuwa ni kipigo cha 1-0 walichopata kutoka kwa Hispania, mwaka 2010. Wanaingia Russia wakiwa wamecheza mechi nane bila kufungwa.

4. NAHODHA ALIYEFUNGA MABAO MENGI

Diego Maradona anashikilia rekodi ya kuifungia Argentina mabao mengi zaidi akiwa na kitambaa cha unahodha. Katika michuano ya mwaka huu, Lionel Messi ambaye wengi wanamfananisha Maradona kiuchezaji, anaenda Russia akiwa na nahodha huku akihitaji mabao matatu tu kufikia rekodi hii.

5. MECHI NYINGI BILA KUFUNGWA KATIKA MICHUANO MIWILI MFULULIZO

Mexico inashikilia rekodi ya kucheza katika mechi tano za Kombe la Dunia, bila kufungwa.

Rekodi hii waliiweka katika michuano ya Kombe la Dunia, iliyofanyika nchini Marekani (1994) na michuano iliyofuata katika ardhi ya Ufaransa, mwaka 1998.

Kuelekea Russia, timu ya taifa ya Costa Rica, ambayo iliingia dimbani katika mechi tano bila kuruhusu nyavu zake kuguswa huko Brazil (2014), wataweza kufikia na kuvunja rekodi hii kama watazuia mabao kutinga katika nyavu zao mwaka huu.

6. MABAO MENGI ZAIDI KATIKA FAINALI TATU TOFAUTI

Thomas Muller anaenda Russia akiwa na malengo makubwa tu. Anataka kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye fainali tatu tofauti.

Muller (28), anahitaji kufunga mabao tano tu, kuwapiku mjerumani mwenzake Miroslav Klose na Teofilo Cubillas wa Peru.

Lakini pia kama atafunga mabao sita, atavunja rekodi mabao mengi ya muda wote (mabao 16 ya Miroslav Klose).

 

7. FAINALI NYINGI ZA KOMBE LA DUNIA

Katika kikosi cha wachezaji 23 cha Mexico, Rafa Marquiz naye yumo.

Unajua maana yake? Hii inamaanisha kuwa, Marquiz anaenda Russia kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza katika michuano mingi ya Kombe la Dunia.

Hii ni michuano yake ya tano kuvaa jezi ya Mexico. Nakuwa nyota wa tatu kufikisha idadi hiyo, akiungana Mmexico mwenzake, Antonio Carbajal na gwiji wa Ujerumani, Lothar Matthaus. Gigi Buffon naye angekuwepo katika orodha hii lakini katika fainali yake ya tano (France, 1998) Buffon aliishia kusugua benchi.

8. SARE NYINGI MARA MBILI MFULULIZO

Belgium wanashikilia rekodi ya kutoa sare katika mechi tano mara mbili mfululizo. Walitoa sare tano kwenye michuano ya Kombe la Dunia, yaliyofanyika nchini Ufaransa (1998) kabla ya kurudia tena kule Korea Kusini (2002).

Costa Rica, wanafukuzia rekodi hii, kwani katika fainali ya mwaka 2014, iliyofanyika nchini Brazil waliambulia sare tano. Mwaka huu, wanaenda Russia wakiwa na matumaini ya kufanya vyema zaidi, lakini wakitoa sare tano, ujue wameweka rekodi!

9. KUFUNGA BAO KATIKA FAINALI NNE TOFAUTI

Tim Cahill (Australia), Rafa Marquez (Mexico) na Cristiano Ronaldo (Ureno), wanahitaji kufunga bao huko Russia kuvunja rekodi ya sasa na kuweka rekodi ya kufunga bao katika fainali nne tofauti za Kombe la Dunia.

Rekodi ya sasa ya kufunga bao katika fainali tatu mfululizo, inashikiliwa na Marquiz, Ronaldo, Cahill, Uwe Seeler, Pele na Miroslav Klose.

10. KUTWAA KOMBE LA DUNIA KAMA MCHEZAJI NA KOCHA

Kila mtu anaitabiria Ufaransa ubingwa mwaka huu, akiwemo Zinedine Zidane. Hata hivyo, kitu ambacho wengi hawakijui ni kwamba, kama hili litatokea, Didier Deschamps ataingia katika vitabu vya historia.

Ubingwa wa Ufaransa, utamfanya aungane na Mario Zagallo na Franz Beckenbauer, katika orodha ya watu waliotwaa kombe hili wakiwa wachezaji na kisha baadaye wakiwa makocha. Deschamps alikuwa nahodha wa France walipobeba ndoo mwaka 1998.