Real, Man Utd, City kuliamsha dude Ulaya

Muktasari:

Real Madrid ni mabingwa mara 13 wa Ligi ya Mabingwa na fainali za msimu huu zitafanyika kwenye uwanja wao

Madrid, Hispania. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid, wanachekelea kupangiwa mwamuzi mwenye bahati nao wanapoanza kampeni ya kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha AS Roma ya Italia katika mchezo wa kwanza wa kundi G.

Shirikisho la soka Ulaya (Uefa) limemteua mwamuzi Bjorn Kuipers wa Uholanzi kuchezesha pambano hilo, huku akionekana kuwa na bahati sana na Madrid jambo lililowafurahisha mashabiki wa klabu hiyo.

Wakati Real ikiialika Roma kwenye dimba la Santiago Bernabeu, mjini Madrid, mwamuzi huyo atakuwa akiichezesha kwa mara ya sita kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kati ya mara tano alipoichezesha timu hiyo iliibuka na ushindi michezo minne na kutoka sare mmoja.

Alianza kuichezesha Real katika msimu wa 2011/12 mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora walipocheza na CSKA Moscow ya Russia na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Moscow.

Alichezesha tena katika msimu wa 2012/2013 katika nusu fainali dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, kwenye uwanja wa Signal Iduna Park na Real ikashinda kwa mabao 4-1, akachezesha tena msimu wa 2013/14 mchezo wa fainali walipoishinda Atlético Madrid mabao 4 -1.

Mara mbili za mwisho aliichezesha mwaka jana kwenye hatua ya makundi ilipoicharaza kwa mabao 3-1 Borussia Dortmund na katika nusu fainali dhidi ya Bayern Munich mjini Munich na Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa mwamuzi huyo katika michuano hiyo kwa msimu huu wa 2018-19 na Real itakuwa ikianza kulisaka taji la 14 la michuano hiyo mikubwa zaidi kwa klabu barani Ulaya, ikiwa ndiyo klabu inayoongoza kulitwaa mara nyingi zaidi.

Pamoja na Real kumfurahia zaidi Kuipers kutokana na kuwa na bahati nao lakini bado pia Roma watafurahia uamuzi wake kwani amekuwa hana tabia ya kuvuruga mechi kwa kuwatoa wachezaji mchezoni kwa kadi za mara kwa mara.

Mechi nyingine za Ligi ya Mabingwa Ulaya leo timu ya kwanza ikiwa mwenyeji: Shakhtar Donetsk vs TSG 1899 Hoffenheim, Ajax vs AEK Athens, Manchester City vs Olympique Lyon, Viktoria Plzen vs CSKA Moskva, Benfica vs Bayern Munchen, Young Boys vs Manchester United na Valencia vs Juventus.

&&&&&