Rashford hatihati kucheza Kombe la Dunia

Wednesday June 13 2018Marcus Rashford.

Marcus Rashford. 

London, England. Kocha wa England, Gareth Southgate amesema hataki kucheza kamari kwa kumtumia mshambuliaji kinda Marcus Rashford katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Tunisia.

Mshambuliaji huyo wa Manchester United, amekwenda Russia akiwa na jeraha la goti aliloumia wakati wa mazoezi kwenye Uwanja wa St George Park, London.

Rashford leo anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu jeraha hilo kabla ya kuanza fainali hizo ambazo ufunguzi wake utafanyika kesho mjini Moscow.

Southgate alidokeza ingawa kinda huyo alicheza vyema mechi ya mwisho dhidi ya Costa Rica wiki iliyopita, lakini anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Kocha huyo atalazimika kumbadili namba kiungo wa pembeni Raheem Sterling kucheza pacha na nahodha Harry Kane katika safu ya ushambuliaji.

Kane anayecheza fainali zake za kwanza za Kombe la Dunia, alisema wamejiandaa vyema kwa michuano hiyo inayomalizika Julai 15.

“Tutamungalia kwa karibu kesho, kila kitu kitakuwa wazi. Lakini wachezaji wote walikuwa fiti kwa takribani wiki tatu zilizopita na wote 23 walinya mazoezi kwa kiwango bora,” alisema Southgate.