Rais Shein aipongeza Z’bar Heroes

Muktasari:

  • Z’bar inasaka ubingwa wa pili wa Kombe la Chalenji  tangu ilipotwaa taji hilo 1995

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepokea kwa furaha kubwa matokeo ya ushindi wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Zanzibar “Zanzibar Heroes” katika mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoendelea nchini Kenya.

 Kutokana na matokeo hayo Rais Dk. Shein ametoa pongezi zake za dhati kwa wachezaji wote wa timu ya Zanzibar Heroes pamoja na viongozi wao kwa mafanikio makubwa waliyoiletea Zanzibar hadi kufika fainali.

 Dk. Shein alieleza kuwa, kwa hakika ushindi wa Timu ya Zanzibar ni ushindi wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla na umeiweka Zanzibar kwenye kiwango kizuri katika ramani ya michezo katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati na nje ya mipaka ya Tanzania.

 “Natoa pongezi za dhati kwa wachezaji wote wa “Zanzibar Heroes” pamoja na viongozi wao kwa mafanikio makubwa waliyotuletea hadi kufikia hatua ya fainali ya mashindano hayo”,alisema Dk. Shein.

 Aidha, Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya timu ya Zanzibar Heroes kushinda katika mchezo wa fainali kutokana na uwezo mkubwa walioonesha vijana wetu kwenye mashindano hayo.

 Dk. Shein alieleza kuwa Serikali na wananchi wote, wako pamoja na timu hiyo pamoja na viongozi wao kwa hali na mali katika kuhakikisha wanarudi na ushindi.

 Sambamba na hayo, salamu hizo za pongezi alizozitoa Dk. Shein zilieleza kuwa maandalizi ya kuwapokea na kuwarudisha nyumbani yameshaanza kupitia uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.

Dk. Shein aliwataka wananchi wote wa Tanzania kuungana kwa pamoja kuwaombea dua na kuwatakia kila la kheri katika mchezo wa kesho wa fainali watakapocheza na timu ya Harambee Stars ya Kenya.

 Timu ya Zanzibar Heroes imetinga fainali za michuono hiyo ya Chalenji baada ya kuifunga Uganda mabao 2-1 na kuivua ubingwa katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana uwanja wa Moi uliopo Kisumu, Kenya.

 Kutokana na matokeo hayo Zanzibar Heroes sasa itacheza fainali za mashindano hayo kwa kuwavaa wenyeji Kenya katika mchezo utakaofanyika kesho Jumapili.

Kenya ilitinga fainali hizo baada ya kushinda  bao 1-0, dhidi ya Burundi katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyofanyika juzi.