Rage ahitaji muda kuijua Katiba mpya Simba

Muktasari:

Rage ameahidi kutenga muda wa kuisoma vizuri katiba hiyo,  ili aweze kuielewa vizuri na kujua faida zake kwa wanachama na klabu kwa ujumla ndiyo aweze kuichambua.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusu uamuzi uliofikiwa na timu ya Simba, hadi apate muda wa kuipitia Katiba mpya ya timu hiyo iliyopitishwa.Katiba hiyo inaelezea mfumo wa uendeshaji wa timu hiyo.

Rage ameahidi kutenga muda wa kuisoma vizuri katiba hiyo,  ili aweze kuielewa vizuri na kujua faida zake kwa wanachama na klabu kwa ujumla ndiyo aweze kuichambua.

Ametolea mfano wa CCM zamani walianzisha kitu kilikuwa kinaitwa Sukita na ilipofilisika, CCM iliendelea kubaki na kwamba jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa kina kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Inadaiwa kuwa, miongoni mwa vipengele vipya ambavyo vipo katika katiba hiyo ni mwanachama mpya anatakiwa kununua hisa kwa gharama ya Sh400,000.

Hali hiyo, imesababisha Rage kuhoji kama walishindwa kuchangia Sh1,000, wanawezaje kutoa kiasi hicho.

"Sipendi kuzungumzia kitu chochote juu ya katiba na mpango huo wa hisa kitu ambacho sijakisoma kwa kina,  ila kama ni kweli sijui maana yake nini. Ngoja niisome katiba hiyo kwa kina ndipo naweza nikaielezea kwa kina," alisema Rage.