RT yampa kisogo Sulle

Muktasari:

Mwanariadha huyo alijiondoa katika kambi ya timu ya taifa kwa madai ni mgonjwa


Arusha: Sakata la mwanariadha Agostino Sulle linazidi kuwa tete baada ya viongozi wa Shirikisho la Riadha Nchini (RT) kusema jambo hilo halina haraka.

Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya RT, Christian Matembo alisema anasubili viongozi wake wampe mwongozo kuhusu mwanariadha huyo aliyeonesha utovu wa nidhamu katika kambi ya Taifa.

“Anayeitisha vikao vyote vya RT ni katibu Mkuu, hivyo tangu aondolewe kambini mwanariadha huyo hakuna kikao kilichokaliwa na kulijadili suala hilo na hakuna mtu mwingine mwenye mamlaka ya kuitisha kikao zaidi ya katibu,” alisema Matembo.

Aliongeza kuwa hawezi kusema ni adhabu gani atakayeweza kukumbana nayo Sulle licha ya sheria za Shirikisho kuwa wazi hivyo inategemea na maelezo atakayotoa mwanariadha siku ya kulijadili jambo lake kama Katibu ataliitisha kikao.

 Hata hivyo katibu mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alipouliuzwa alisema bado jambo hilo halijajadiliwa kwa kuwa akili ya viongozi wote kwa sasa ipo kwenye mashindano yaliyopo mbele yao.

 “Siwezi kukueleza tutakaa lini kwa maana wiki hii nitasafiri kwenda Hispania kuhudhulia mkutano mkuu wa kanda utakaofanyika siku moja kabla ya mashindano ya Dunia ya nusu marathon yatakayofanyik Aprili 24” alisema Gidabuday.

Alisisitiza mwanariadha huyo hataruhusiwa kujihusisha na riadha hadi pale shauri lake litakaposikilizwa, hivyo kama watalijadili baada ya kutoka Hispania au baada ya kurejea Australia kwenye mashindano ya jumuiya ya Madola hilo halijajulikana kwa sasa.