Profile yagawa dozi Ligi ya kikapu Mwanza

Muktasari:

  • Mchezo kwa timu hizo ulikuwa wa raundi ya nne ambapo Profile mabingwa watetezi wa Ligi hiyo haijapoteza hata mmoja na kuendelea kujikita kileleni, huku Eagle wakishika nafasi ya nne.

Mwanza. Profile si ya mchezo mchezo kabisa kwenye Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza baada ya kuiangushia kipondo kikali Eagles cha pointi 71-50 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mirongo, Mwanza.

Mchezo kwa timu hizo ulikuwa wa raundi ya nne ambapo Profile mabingwa watetezi wa Ligi hiyo haijapoteza hata mmoja na kuendelea kujikita kileleni, huku Eagle wakishika nafasi ya nne.

Katika mchezo huo ulishuhudiwa na mashabiki wengi kutokana na ushindani unaokuwapo kwa timu hizo pindi zinapokutana, Profile iliwazidi wapinzani hao dakika za mwisho na kuweza kuondoka na ushindi.

Mchezaji Amon Sembeye alifunga pointi 16 ikiwamo ya mitupo ya mbali timu yake ya Profile, huku Makulu Francis yeye akiiwekea wavuni pointi 15.

Nahodha wa Eagle, Laurent Masatu alisema licha kuanza vyema lakini walijikuta wakikata pumzi dakika za mwisho pamoja na mwanga wa taa za usiku ukawachanganya zaidi.

“Kama uliona raundi tatu tulikuwa vizuri lakini ngwe ya mwisho tukakata pumzi kwa sababu ya huu mwanga wa taa hizi za usiku,tutaendelea kupambana katika mechi zilizobaki”alisema Masatu.

Kamishna wa ufundi na uendeshaji wa Chama cha mchezo huo Mkoa wa Mwanza (MRBA), Aidari Abdul alisema kuwa kutokana na ushindani kwa timu ulioonekana msimu huu imewalazimu kutumia waamuzi watatu ili kuondokana na malalamiko.

Alisema MRBA inaamini bingwa atakayepatikana atakuwa bora na mwenye uwezo wa kushindana hata kwenye mashindano ya kimataifa na kuwakilisha vyema Mkoa.