Prisons waivutia nguvu Abajaro

Muktasari:

Katibu wa Prisons, Havimtishi Abdallah amesema, watacheza mechi tofauti za kirafiki zitakazowaandaa kucheza mashindano FA.

KIKOSI cha Tanzania Prisons cha Mbeya kimeanza kujifua kwa ajili ya michuano ya  Kombe la FA inayotarajiwa kuanza rasmi Desemba 20 mwaka huu ambapo wao watafungua dimba na Abajaro ya Daraja la Kwanza.

Kwa mujibu wa katibu wa timu hiyo, Havimtishi Abdallah amesema, watacheza mechi tofauti za kirafiki zitakazo waandaa kwa ajili ya mashindano hayo ambayo Simba ndiyo bingwa mtetezi.

"Lazima tujipange kikamilifu, kwani anayekuwa bingwa wa  FA, anapata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa,kama ilivyo kwa Simba ambao walifanikiwa kutwaa ubingwa mwaka jana baada ya kuwafunga Mbao FC,"anasema Havimtishi.

Kuhusu usajili amesema, wanatarajia kumalizana na kipa ambaye wanamchukua kutoka Ligi Daraja la Kwanza na straika wa Ligi Daraja la Pili, kutoka Zanzibar, huku akisisitiza watayaanika majina yao, kila kitu kikikaa sawa.

"Bado hatujafikiana nao mwafaka, ndio maana tunashindwa kuwaweka wazi, ila tutasajili kutoka kwenye ligi ya madaraja ya chini,tunaamini wana uwezo watatuongezea nguvu katika ligi na Kombe la FA,"anasema.