Poulsen amtia ndimu mbongo anayekipiga Ujerumani

Muktasari:

  • Poulsen ni mchezaji mwenye asili ya Tanzania, lakini yupo katika kikosi cha Denmark kinachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Russia.

Dar es Salaam. Beki Emily Mgeta anayekipiga katika klabu ya VfB Eppingen inayoshiriki Ligi Daraja la Tano nchini Ujerumani,  amejikuta akikoshwa  na mafanikio aliyoyapata Mbongo mwenzake Yusuf Poulsen ambaye anakitumikia kikosi cha timu ya Taifa ya Denmark.

Poulsen ni mchezaji mwenye asili ya Tanzania, lakini yupo katika kikosi cha Denmark kinachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Russia.

Amesema, mchezaji huyo ni kati ya wachezaji ambao wamepambana kwa muda mrefu, mpaka hivi sasa amefanikiwa kuonekana na kujulikana dunia nzima.

“Namjua akiwa Ujerumani tangu Ligi Daraja la Tatu, anajua kupambana kiukweli na aliweza kukomaa na timu yake tangu ikiwa ipo Ligi Daraja la Tatu mpaka anafanikiwa kufika ligi kuu, naamini na mimi nitafika kwa sababu njia ndiyo zile zile,” amesema.

Akizungumzia kuhusu kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania, amesema yupo na amekuwa akiwasiliana na viongozi wa TFF mara kwa mara kuhusu Taifa Stars.

“Niliwahi kuzungumza na aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuhusu kuja kucheza Taifa Stars, lakini mambo yaliingiliana nikashindwa kujiunga nao,” amesema.