Mourinho ajivunia kurudi kwa Pogba

Muktasari:

  • Kiungo huyo Mfaransa aliumia mwezi uliopita wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Manchester, England.Kocha Manchester United, Jose Mourinho ni mwenye furaha baada ya taarifa kuweka wazi kiungo wake Paul Pogba atakuwa fiti kuzivaa Arsenal na Manchester City.

Pogba yupo nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi sasa huku akitarajiwa kuwa fiti kuanza kucheza mechi itakapofika Desemba.

Habari njema kwa kocha Mourinho ni kwamba Pogba atarudi katika mwezi ambao kawaida umekuwa na mechi nyingi sana zinazotoa mwanga wa kutambua mbio za kuwania ubingwa zilivyo.

Man United itakipiga na Arsenal, Desemba 2 huko uwanjani Emirates na siku nane baadaye, yani Desemba 10 watakuwa Old Trafford kuwakaribisha mahasimu wao wakuu, Man City.

Man United jana Jumamosi ilikubali kipigo cha kwanza kwenye Ligi Kuu England ilipochapwa na Huddersfield na kichapo hicho kinawafanya waachwe kwa pointi tano na wapinzani wao katika mbio za michuano hiyo, Man City.