Wachezaji Singida wampa raha Pluijm

Muktasari:

Pluijm kocha wa zamani wa Yanga, tangu ajiunge na Singida alianza michuano ya Ligi Kuu Bara kwa kusuasua lakini mwenendo wa kikosi chake kwa sasa unampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi.

KOCHA wa Singida United, Hans Pluijm anapata raha kwa sababu timu yake imekuwa ikifanya vizuri kila siku zinapoongezeka na katika usajili wa dirisha dogo, upo uwezekano akafanya mabadiliko kwa wachezaji wa kigeni.
Pluijm kocha wa zamani wa Yanga, tangu ajiunge na Singida alianza michuano ya Ligi Kuu Bara kwa kusuasua lakini mwenendo wa kikosi chake kwa sasa unampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi.
"Kwa sasa hali ni nzuri na kuna matumaini makubwa kwani kila siku zinavyosonga mbele ndivyo wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri na kushika zaidi,"alisema Pluijm.
Akizungumzia mpango wa usajili wake kwenye dirisha dogo Pluijm alisema, atakuwa na majibu mazuri baada ya mchezo wao ujao na Mbeya City.
"Bado nina mchezo, tutakapomaliza na Mbeya City, ndiyo naweza kuzungumza zaidi na hiyo baada ya kukaa na uongozi wangu, mabadiliko yanaweza kuwepo labda kwa wachezaji wa kigeni,"alisema.
Katika msimamo wa ligi,  Singida United ipo nafasi ya tano na pointi 17  ambazo ni sawa na za Mtibwa Sugar iliyo nafasi ya nne, Simba ndiyo vinara wana pointi 22, sawa na Azam FC iliyo ya pili wakitofautina kwa idadi ya mabao na Yanga ni ya tatu ina pointi 20.