Pluijm aitolea macho Biashara United

Muktasari:

  • Hii ni mara ya kwanza kwa Azam kucheza dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Karume, Mara

Dar es Salaam. Kocha wa Azam, Hans Van Der Pluijm, amesema hasira za kuambulia pointi moja dhidi ya Mwadui, zitaishia kwa Biashara United.

Azam inateremka dimbani kesho kuwania pointi tatu, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Pluijm, alisema hakuridhika na matokeo ya sare na Mwadui kwa kuwa timu yake ilistahili kupata pointi tatu katika mchezo huo.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga na Singida United, alisema mabeki walizembea kuokoa hatari langoni mwao na kusabanisha Mwadui kupata bao.

Alisema dakika moja iliwaponza baada ya Mwadui kutumia nafasi kupata bao la kusawazisha na kuipoka pointi mbili ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi saba, itakuwa na kazi ngumu kupata ushindi baada ya kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar kwenye uwanja wao.

Pluijm raia wa Uholanzi ametoa maelekezo kwa wachezaji wake akiwataka kutumia mbinu na mafunzo aliyowapa kupata ushindi.

"Tunatakiwa kutumia vizuri kila nafasi tunayopata ili kupata mabao, najua tuna uzoefu zaidi ya wapinzani wetu na tunawapa heshima zote, lakini tutacheza kwa nguvu hatutaki tena kupoteza pointi katika mchezo huo,"alisema Pluijm.