Pluijm achimba mkwara

Hans Van Pluijm

SI unajua kocha Hans Van Pluijm aliondoka kimizengwe pale Jangwani. Sasa kocha huyo ambaye anakinoa kikosi cha Singida United, amechimba mkwara mzito kwa waajiri wake wa zamani.

Pluijm ametamba kuisambaratisha Yanga na kuitupa nje kwenye robo fainali ya Azam Federation Cup, ili kikosi chake kisonge mbele.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mdachi huyo amesema kikosi chake kinajifua ili kupata matokeo mazuri tena kwa mabao ya mapema.

“Wachezaji wapo kambini lakini kuna baadhi hawatakuwepo ila haliwezi kutupa taabu kwa sababu lengo letu ni tupate matokeo kwenye mechi zozote tunazokutana nazo kuanzia sasa,” alisema.

Alisema mchezo huo utakuwa kama fainali kutokana na ubora wa timu zote, lakini akaingiwa hofu na Yanga ambao wametoka kwenye mchezo wa kimataifa dhidi ya Townsdhip Rollers ya Botswana.

“Tunataka kupata matokeo mazuri na hilo ndio lengo letu, japo Yanga wametoka kwenye mashindano makubwa hivyo, ni faida kwao lakini vijana wangu wako tayari kwa mapambano,” alisema.