Beki tatizo jipya Man City

Muktasari:

Kocha huyo anataka libero mpya baada ya nahodha Vincent Kompany kuwa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la misuli na John Stones ni majeruhi.

London, England. Pep Guardiola amelazimika kuwashawishi mabosi wa Manchester City kuingia sokoni kusaka beki mpya wa kati katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Kocha huyo anataka libero mpya baada ya nahodha Vincent Kompany kuwa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la misuli na John Stones ni majeruhi.

Guardiola amelazimika kumtumia beki wa akiba Eliaquam Mangala katika mechi za hivi karibuni kujaza nafasi ya Stones. Kocha huyo anataka mchakato huo kukamilika mwezi ujao.

Macho ya kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich yametua kwa libero wa Southampton, Virgil van Dijk au Jonny Evans wa West Ham Bromwich.

Van Dijk alishindwa kutua Liverpool majira ya kiangazi msimu uliopita baada ya kuwekwa sokoni kwa Pauni 70 milioni, hivyo Man City italazimika kuvunja benki.