Pep apata ufumbuzi wa timu yake

Muktasari:

  • Cristina amekuwa akiishi na Pep kwa muda mrefu kiasi cha kutosha, hakuhitaji maelezo zaidi, anamjua akiwa katika hali hiyo, akiwa amevurugwa, na mwenye hali ya hofu, ni kwa sababu anakuwa mwenye kujilaumu kwa jambo fulani.

KATIKA toleo lililopita kwenye Kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alilichambua tukio muhimu la Kocha Pep Guardiola pale anapoamua kukaa kutafuta suluhisho katika timu yake hasa anapokuwa nyumbani kwake. Endelea…

Cristina amekuwa akiishi na Pep kwa muda mrefu kiasi cha kutosha, hakuhitaji maelezo zaidi, anamjua akiwa katika hali hiyo, akiwa amevurugwa, na mwenye hali ya hofu, ni kwa sababu anakuwa mwenye kujilaumu kwa jambo fulani.

Hakuwa mwenye fikra za kuwalaumu wachezaji wa Bayern kwa kiwango chao dhaifu, anajilaumu na kujiona anawajibika kwa kushindwa kuwafanya wachezaji watumie ubora wao, kwa kushindwa kupata neno au mazoezi sahihi, kwa kutowaweka katika nafasi sahihi au kuwapa nafasi wajielezee wenyewe.

Pep ni mtoto na mjukuu wa wahangaikaji, kama ambavyo wanaitwa kwa jamii ya watu wa Catalunya yaani mtu wa kujituma katika maisha, baba yake, Valentin ni fundi mwashi katika mji wa Santpedor, Catalunya, amemfundisha mtoto wake kujisimamia mwenyewe na kuwa tayari kuwajibika kwa matendo yake na si kulaumu wengine.

Pep anaweza kuwa miongoni mwa makocha wanaoheshimiwa duniani, ameongoza moja ya klabu kubwa duniani, lakini bado anabaki kuwa ni mtoto wa fundi mwashi ambaye kazi yake ni kujenga nyumba za matofali na ana wajibu wa kuwajibika kwa matendo yake.

Alitumia saa sita akiangalia mechi ya Jumamosi kwenye televisheni kwa kurudiarudia huku akiandika baadhi ya matukio muhimu kwenye kijitabu chake, alikuwa akiyafuta na kuanza kuyafikiria upya.

Fundi mwashi ni mjenzi muungwana, Pep aliendelea kuyachambua na kuyachambua matatizo yale kwa jioni ile na baadaye akapata jibu kisha akaita kwa sauti ya juu, Maria! Marius! Njooni haraka, nimeshapata.

Kelele ile haikuwa ikiashiria hasira bali ni mfano wa mvumbuzi mwanafunzi ambaye alifarijika na kujiona yupo tayari kwa mtihani, ni kilio cha mtu aliyeridhishwa na jambo baada ya kupata suluhisho la tatizo lakini alifahamu bado ana wajibu wa kulipitisha mbele ya walimu wake.

Maria na Marius ndio walimu wake, Pep ana tabia ya kuwaambia kila kitu kuhusu mechi zake na watoto wake hao wanalifurahia jambo hilo, wote ni wapenzi na wanahamasishwa na mambo yanayohusu mbinu za kiuchezaji na zaidi ya hilo hawajawahi kukaa kimya pale wanapofikiri baba yao amekosea lakini jioni ya leo walikubaliana naye na kumpa tano. Amepata alama za ushindi.

Hadi saa mbili asubuhi ya siku iliyofuata, kocha huyu tayari alikuwa amejibanza kwenye ofisi yake ya Sabener Strasse akiwa na Manel Estiarte meza yao ilikuwa imejaa makaratasi na walikuwa wakiiangalia mechi ya Hannover kwenye kompyuta.

Kulikuwa na mbinu nyingi za kiuchezaji zilizoandikwa kwenye ubao mweupe. Estiarte anaikumbuka siku hiyo ya asubuhi kwa tabasamu, “Asubuhi hiyo ilikuwa ni kati ya matukio 10 bora ya Pep na huyu jamaa ana matukio mengi ya kuhamasisha, inafurahisha.

Pep alikuwa juu mfano wa kishada, hofu ya Jumamosi ya kutokwenda sawa na timu ghafla ikageuka na kuwa Jumatatu yenye matumaini baada ya kufanikisha jambo. Alianza kuelezea mawazo yake taratibu na baadaye akaongeza kasi hadi kujikuta akipotea kutokana na namna alivyokuwa akitoa ishara na mifano kwa wingi.

Na hiki ndicho alichokuwa akikifikiria: “Tunamuweka Lahm kwenye kiungo, hilo si jambo linalohitaji mjadala, kwa pande zote mbili wanaomsaidia watakuwa ni Boateng na Dante ili Lahm aweze kuitumia kasi yake kuisumbua timu pinzani.

“Bastian (Shweinsteiger) na Kroos watakuwa mbele viungo washambuliaji kisha tutachambua mwelekeo wa timu, Rafinha na Alaba katika mazingira hayo si tena mabeki wa pembeni, wanaungana kwenye kiungo, kimsingi wanatawala sehemu karibu ya kati ingawa wanaweza kwenda mbele kumsaidia Robben na Ribery kama itakuwa sahihi kufanya hivyo.

Itaendelea Jumamosi ijayo…