Penalti zamnyima Msuva ubingwa

Kuna muda mipango inaweza isiwe matumizi, tulicheza vizuri mwanzo hadi mwisho wa mchezo. Walianza kutufunga kipindi cha kwanza, lakini tulisawazisha kipindi cha pili, kwenye penati tukapoteza, siku zote penati hazina mwenyewe.”

 SIMON MSUVA- DIFAA EL JADIDA

WINGA machachari nchini, Saimon Msuva amepoteza nafasi ya kushinda taji la kwanza nchini Morocco baada ya klabu yake ya Difaa El Jadida kuondolewa kwenye Kombe la Mfalme.

Difaa ilitinga hatua ya fainali baada ya kuifunga RSB Berkane kwa matokeo ya jumla, mabao 4-3.

Raja Casablanca ambao wamechukua ubingwa huo kwa kuifunga timu ya Msuva penalti 3-1, wao walitinga hatua hiyo kwa kuwaondoa FAR RABAT kwa faida ya bao la ugenini.

“Kuna muda mipango inaweza isiwe matumizi, tulicheza vizuri mwanzo hadi mwisho wa mchezo. Walianza kutufunga kipindi cha kwanza, lakini tulisawazisha kipindi cha pili, kwenye penati tukapoteza, siku zote penati hazina mwenyewe.

“Kilichobaki ni kuelekeza nguvu kwenye ligi, kule napo inawezekana tukafanya vizuri japo ingependeza zaidi kama tungeshinda Kombe la Mfalme ila ndiyo hivyo imeshatokea,” alisema Msuva.

Katika mchezo huo Msuva aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Adnane El Ouardy.