#WC2018: Pazia Kombe la Dunia lachanwa hapa!

Muktasari:

Mbali na mechi ya ufunguzi, uwanja huu pia utatumika katika mechi ya fainali ya michuano hiyo. Luzhniki ni uwanja mkubwa kuliko viwanja vyote vitakavyotumika kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Fainali za Kombe la Dunia 2018 zitaanza kutimua vumbi Juni 14, kwa mechi ya ufunguzi kati ya wenyeji Russia dhidi ya Saudi Arabia. Mechi itapigwa kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow.

Mbali na mechi ya ufunguzi, uwanja huu pia utatumika katika mechi ya fainali ya michuano hiyo. Luzhniki ni uwanja mkubwa kuliko viwanja vyote vitakavyotumika kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Uwanja huu una uwezo wa kuchukua watu 81,000 walioketi, ukishika nafasi ya kwanza kwa kuchukua idadi ya watazamaji wengi nchini Russia na unashika nafasi ya nane kwenye barani Ulaya, ukizidiwa na viwanja vya Camp Nou (Hispania 99,354), Wembley (England 90,000), Croke Park (Ireland 82,300), Twickenham (England 82,000), Signal Iduna Park (Ujerumani 81,359), Stade de France (Ufaransa 81,338) na Santiago Bernabeu (Hispania 81,044).

Uwanja huu pia ulitumika kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980 iliyofanyika jijini Moscow, Russia. Pia, uliwahi kutumika katika michezo mikubwa barani Ulaya kama vile Fainali ya Kombe la Uefa ya mwaka 1999 kati ya Olympique Marseille (Ufaransa) na Parma (Italia) na Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008 kati ya Chelsea na Manchester United.

Uwanja huu pia uliwahi kutumika kama uwanja wa nyumbani wa klabu tatu za Jiji la Moscow. Klabu hizo ni CSKA Moscow, Torpedo Moscow na Spartak Moscow, lakini baadaye ulibadilishwa na kuwa uwanja wa taifa na sasa unatumiwa kwa mechi za timu ya taifa ya nchi hiyo.

Uwanja huu upo kwenye Wilaya ya Khamovniki , jimbo la Okrug jijini Moscow. Jina Luzhniki limetokana na eneo la uwanda wa kijani karibu na mto Moskva, ambapo uwanja huo umejengwa. Eneo hilo lilichaguliwa kujenga uwanja huo kutokana na ukubwa na ukaribu kutoka katikati ya jiji hilo.

Mwaka 1980 uwanja huo ulianza kuandaa mashindano makubwa yanayosimamiwa na FIFA pale ulipoanda michezo ya Olimpiki. Mwaka 1982 kwenye mechi ya kombe la Uefa kati ya Spartak Moscow na HFC Haarlem kulitokea maafa makubwa uwanjani hapo na watu 66 walikufa na wengine kujeruhiwa.

Maafa hayo yalipewa jina la ‘Maafa ya Luzhniki’ (Luzhniki Disaster) na yanatajwa kuwa moja ya matukio mabaya zaidi ya kimichezo kuwahi kutokea katika historia ya taifa la Russia.

Baada ya kuchaguliwa kuwa uwanja utakaotumika kwenye mchezo wa mwisho wa Fainali za michuano hiyo, Julai 15 mwaka huu. Uwanja huo utaingia kwenye rekodi ya kuwa miongon i mwa viwanja sita duniani kuwahi kuandaa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, fainali ya Kombe la Uefa, fainali ya ligi ya Mabingwa Ulaya na michezo ya Olimpiki.

Viwanja ambavyo vipo kwenye rekodi hiyo ni Stadio Olimpico (Roma, Italia), Berlin Olympia (Berlin, Ujerumani),  Munich Olympia (Munich Ujerumani), Stade de France (Paris, Ufaransa) na Wembley (London, England).

Mbali na mechi ya ufunguzi na mchezo wa fainali, uwanja huo pia utatumika kwenye mechi mbalimbali za fainali hizo. Jumla ya mechi saba zitachezwa kwenye dimba hilo. Mechi nne ni za hatua ya makundi, mechi moja ya hatua ya 16 bora, mechi moja ya hatua ya nusu fainali na mechi ya fainali.

Kwa ujumla, Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia zitatumia viwanja 12 ambavyo ni: Luzhniki, Otkrytiye, Krestovsky, Kaliningrad, Kazan, Nizhny Novgorod, Cosmos, Volgograd, Mordovia, Rostov, Fisht na Central.