Pasi Kali za Mabao

Muktasari:

  • Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Mohamed Salah na Harry Kane wanaweza kuwa ni hatari kwenye kutupia mipira wavuni, lakini nyuma yao kuna watu matata, ambao waliwapigia pasi na kufunga kirahisi sana.

LONDONENGLAND

KWENYE mechi za soka wanasifika sana wafungaji, lakini asikwambie mtu, mwogope sana anayetoa pasi ya mwisho ya kabla ya bao halijafungwa, hao ndio watu wanaotisha kwenye soka la kisasa.

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Mohamed Salah na Harry Kane wanaweza kuwa ni hatari kwenye kutupia mipira wavuni, lakini nyuma yao kuna watu matata, ambao waliwapigia pasi na kufunga kirahisi sana.

Hizo pasi kwenye soka zinaitwa asisti na kuna wakali matata kabisa wanaopiga asisti, ambazo zinamwacha mfungaji yeye na nyavu tu au yeye na kipa tu kama anayepiga penalti.

Hawa hapa waliofunika kwa kupiga pasi nyingi za mabao kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kuwa gumzo kwa mashabiki wote kutokana na mipira waliyopiga bila kujali wafungaji wa mabao hayo wamefunga katika staili ya aina gani.

Kevin de Bruyne - asisti 15

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne anacheza soka la ubora wake na kuwa gumzo kila mtaa. Amekuwa staa asiyeshikika uwanjani, lakini kubwa ambalo limekuwa likiwatesa wapinzani ni uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho ambazo zimekuwa zikiwarahisishia kazi ya kufunga kina Sergio Aguero na mwenzake Gabriel Jesus.

Katika Ligi Kuu England msimu huu, Mbelgiji huyo amepiga pasi 2,401, lakini pasi 15 ndizo kali zaidi ambazo zilileta mabao ya moja kwa moja.

Leroy Sane - asisti 12

Mjerumani Leroy Sane anayecheza soka la ubora mkubwa sana huko Etihad anakoitumikia Manchester City ya Kocha Pep Guardiola. Msimu wake umekuwa mzuri na kuwa miongoni mwa wachezaji waliochangia kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kubeba ubingwa.

Katika msimu huu, Sane ni mmoja kati ya wachezaji wanaoshika nafasi za juu kabisa za kupiga pasi nyingi za mabao baada ya kufanya hivyo mara 12 na kuisaidia timu yake kupata mabao ya kutosha yanayowafanya wanyakue ubingwa wa ligi hiyo bila ya presha yoyote.

David Silva - asisti 11

Unaweza kuona sababu moja kubwa ambayo inafanya Man City kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kuwa ina mafundi wengi wa kupiga pasi za mwisho za mabao ambazo zinafanya timu hiyo kuzoa ushindi kwenye mechi muhimu.

Kwa msimu huu kwenye ligi hiyo, kiungo huyu fundi wa mpira kutoka Hispania, amepiga jumla ya pasi 2,207 ndani ya uwanja, lakini pasi zake 11 zilileta mabao ya moja kwa moja kwenye kikosi hicho chenye maskani yake huko Etihad, ambacho hadi sasa kimevuna pointi 87 na kutangaza ubingwa.

Dele Alli - asisti 10

Kuna kipindi fulani katika msimu huu, staa wa Tottenham Hotspur, Dele Alli alidaiwa kushuka kiwango chake baada ya kuonekana kucheza ovyo kwenye baadhi ya mechi na wengi wakimkosoa wakidai amekuwa akijiangusha sana uwanjani.

Lakini takwimu za mechi hizo zinaonyesha wazi Dele ni miongoni mwa mastaa wanne wa juu waliopiga pasi nyingi za mabao kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Staa huyo ambaye jina lake linahusishwa sana na mpango wa kuondoka kwenye kikosi cha Spurs, amehusika kwenye mabao 10 yaliyotokana na pasi zake za mwisho.

Paul Pogba - asisti 9

Mchezaji ghali kabisa kwenye Ligi Kuu England. Paul Pogba alitua Manchester United akitokea Juventus kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2016 kwa ada ya Pauni 89 milioni.

Wakati akishikilia rekodi hiyo kwenye ligi hiyo, Pogba amekuwa na mchango pia kwa timu yake ambapo kwenye Ligi Kuu England msimu huu amehusika kwenye mabao tisa yaliyotokana na pasi zake za mwisho.

Kwa jumla, Pogba amepiga pasi 1,455 kwenye mechi za ligi, lakini kati ya hizo, pasi tisa zilikuwa matata na kuleta mabao ya moja kwa moja kwa kikosi cha Jose Mourinho.

Christian Eriksen - asisti 9

Kazi ya Kane kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur ni kufunga, lakini kuna wale wengine wenye kazi ya kumlisha mshambuliaji pasi matata zinazompa urahisi wa kusukumia wavuni na hao wachezaji miongoni mwao ni Christian Eriksen.

Kwa msimu huu, Eriksen amecheza mpira mkubwa sana na hakika ya moja kwa moja amekuwa na mchango wa maana kwa timu yake na kufanikiwa kuwamo ndani ya Top Four hadi sasa.

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Eriksen amepiga pasi 2,005, lakini tisa zilikuwa pasi penalti, ambazo ziliwafikia wenzake na kutupia tu mipira wavuni moja kwa moja.

Henrikh Mkhitaryan - asisti 9

Kwa msimu huu, staa wa kimataifa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan alipita kwenye timu mbili, Manchester United kisha Arsenal alikojiunga kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa.

Huduma ya staa huyo si mchezo na ndiyo maana Kocha Arsene Wenger aliamua kumwaacha Alexis Sanchez ili kumchukua mchezaji huyo kwa kubadilishana na Jose Mourinho huko Manchester United.

Kwenye Ligi Kuu England hadi ilipofikia sasa, bila ya kuhusisha mechi za jana, staa huyo alihusika kwenye mabao tisa yaliyotokana na pasi zake za mwisho, ambazo zimewafanya washambuliaji kama Pierre-Emerick Aubameyang kufunga kirahiiisi.

Mohamed Salah- asisti 9

Kitu ambacho Mohamed Salah anakikosa kwenye kikosi chake cha Liverpool kwa msimu huu ni ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini mengine yote yamekwenda vizuri.

Kwanza, ukija upande wa kufunga, staa huyo ndiye kinara, akiwa amepachika wavuni mara 30 kwenye ligi hiyo kabla ya mechi za usiku wa jana.

Lakini, kuonyesha Liverpool inahitaji zaidi huduma yake kwenye ligi ya msimu huu, Mo Salah amehusika pia kwenye mabao mengine tisa yaliyotokana na pasi zake za mwisho alizowapigia wenzake kama Sadio Mane na Roberto Firmino kupasia nyavuni.

Kwa jumla kwenye ligi ya msimu huu, Salah amepiga pasi 864, lakini tisa zilikuwa matata kwa sababu zilileta mabao ya moja kwa moja kwa Liverpool.