Panone Fc yabadili jina sasa ni Kilimanjaro Heroes

Arusha: Uongozi wa Panone FC inayojiandaa na ligi daraja la Pili (SDL) unatarajia kukutana Jumapili kujadili juu ya mabadiliko ya jina la timu hiyo kutokana na masharti waliyopewa na aliyekuwa mfadhili wao.

Katibu Mkuu wa Panone, Augustino Mwakatumbula alisema kwa muda mrefu timu hiyo ilikuwa inafadhiliwa na Patrick Ngiloi ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya Panone, aliyeipa timu hiyo ikapewa jina la Panone Fc.

  “Tumependekeza timu hiyo iitwa Kilimanjaro Heroes na tayari kila kitu kimeenda sawa hata TFF tumepeleka taarifa japo kuna vitu havijakaa sawa ila kila kitu kwa sasa kinatambulika kwa jina la Kilimanjaro Heroes na siyo Panone kama awali ilivyokuwa, hii ni pamoja na mikataba na nyaraka za timu,” alisema Mwakatumbula.

 Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yatawaumiza baadhi ya watu ikiwa pamoja na mashabiki wa timu hiyo yenye maskani yake Mkoani Kilimanjaro, lakini hakuna njia nyingine zaidi ya kubadilisha jina.

Taarifa kutoka kwa wadau wa soka mkoani humo zinaeleza kuwa kujiondoa kwa mfadhili huyo ni kutokana na baadhi ya viongozi wa timu waliokuwa madarakani kutumia vibaya jina la timu kwa kujipatia fedha kwa matumizi yao binafsi jambo ambalo halikumfurahisha tajiri huyo anayemiliki vituo vya mafuta.