PSG inavyoburuza vigogo kwa kulipa mishahara mikubwa

PARIS, UFARANSA. PESA inaongea. Mafanikio ambayo klabu ya PSG inaanza kuyapata sasa hivi ni wazi kwamba, yametokana na kiasi kikubwa cha uwekezaji walichofanya klabuni kwao. Na sasa imegundulika kuwa PSG wanaongoza kwa kulipa wachezaji wao mishahara mikubwa zaidi kuliko klabu yoyote barani Ulaya.

Paris Saint-Germain ( £279m)

(Anayeongoza: Neymar, £537,000-kwa wiki)

Na sasa tuna klabu mpya ambayo inaongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa zaidi barani Ulaya. Ni PSG. Baada ya kumnunua staa wa Brazil, Neymar kwa rekodi ya uhamisho ya dunia kutoka Barcelona kwa dau la pauni 198 milioni, PSG wanamlipa Neymar kiasi cha pauni 33 milioni kwa mwaka na kwa kiasi kikubwa kiasi hicho kimeifanya iwe klabu inayolipa mishahara mikubwa zaidi barani Ulaya.

Kwa sasa ndani ya msimu mmoja wanalazimika kulipa kiasi cha pauni 279 milioni kama mishahara kwa mastaa wao akina Neymar, Edinson Cavani, Kylian Mbappe, Angel Di Maria na wengineo.

Barcelona ( £264m)

(Anayeongoza : Lionel Messi, £500,000 kwa wiki)

Msimu uliopita Barcelona walikuwa wanaongoza kwa kulipa mishahara mikubwa hasa baada ya kumiliki mastaa watatu wakubwa kwa mipigo. Walikuwa wanawamiliki, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Lakini sasa kuondoka kwa Neymar kumepunguza idadi ya noti wanazopeleka benki kila wikiendi. Kwa sasa wanashika nafasi ya pili nyuma ya PSG huku wakilipa kiasi cha pauni 264 milioni kwa mwaka.

Manchester United (£264m)

Anayeongoza Paul Pogba, £290,000 kwa wiki)

Baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson na timu kuyumba katika mikono ya David Moyes, Manchester United imetumia nguvu kubwa ya pesa katika zama za Louis van Gaal na Jose Mourinho. Mpaka sasa mambo hayajakaa sawa vizuri, lakini wao na Barcelona wanashika nafasi ya pili kwa kulipa mishahara mikubwa. United nao wanalipwa pauni 264 milioni kwa mwaka huku kiungo wao, Paul Pogba akiwa analipwa zaidi ya wenzake. Anachukua pauni 290,000 kwa wiki.

Chelsea (£250m)

(Anayeongoza Eden Hazard, £200,000- kwa wiki)

Mafanikio ya Chelsea msimu uliopita hayakuja bure. Yamekuja kutokana na uwekezaji wa muda mrefu wa tajiri, Roman Abramovich. Wanashika nafasi ya nne kwa timu ambazo zinalipa mishahara mikubwa Ulaya. Kuondoka kwa Diego Costa hakujawapa nafuu Chelsea kwa sababu wameingia akina Alvaro Morata na Tiemoue Bakayoko ambao nao wanachukua pesa ndefu. Chelsea inalipa kiasi cha pauni 250 milioni kwa msimu kwa ajili ya mishahara tu.

Manchester City (Pauni 244m)

(Anayeongoza: Sergio Aguero, £220,000- kwa wiki)

Gharama za kumpa kila kitu ambacho Pep Guardiola anataka kwa ajili ya kuisuka upya Manchester City zinaonekana wazi kwa jinsi ambavyo viwango vya matumizi vimepanda Etihad. Katika msimu wa kwanza tu wa Guardiola, City walitangaza kuwa mishahara ya wachezaji wake imepanda kwa asilimia 25.

Hiyo ilikuwa kabla ya kuwasili kwa Benjamin Mendy, Danilo na Kyle Walker, huku Samir Nasri, Joe Hart, Fernando na Wilfried Bony wakiwa klabuni. Na sasa, City inashika nafasi ya tano kwa kulipa mishahara mikubwa barani Ulaya nyuma ya watani zao Manchester United. Matajiri wa kiarabu wa City wanalipa kiasi cha pauni 224 milioni kwa mwaka kwa ajili ya kuwamudu mastaa wao wa bei mbaya.

Real Madrid (Pauni £240 m)

(Anayeongoza Cristiano Ronaldo, £365,000 kwa wiki)

Usitishike sana na Real Madrid. Wanaye Cristiano Ronaldo, ambaye analipwa dau kubwa sana lakini mastaa wengine hawalipwi pesa nene. Madrid wanashika nafasi ya sita nyuma ya PSG, Man United, Man City na Chelsea licha ya kumlipa Ronaldo kiasi cha pauni 365 milioni kwa mwaka. Kuondoka kwa Alvaro Morata kwenda Chelsea na Danilo aliyekwenda Manchester City kumezidi kuwapunguzia mzigo wa mishahara. Tatizo ni kwamba kwa sasa hawafanyi vizuri katika Ligi na kuna uwezekano wakaingia sokoni kwa vurugu msimu ujao na kupandisha dau lao la mishahara.

Bayern Munich (Pauni 235 m)

(Anayeongoza: Robert Lewandowski, 160,000 kwa wiki)

Kwa Ujerumani inabakia kuwa timu tishio na tajiri sana, lakini kwa Ulaya Bayern wanashika nafasi ya saba. Dau lao la mshahara kwa mwaka limeongezeka na zaidi baada ya ya kumchukua kwa mkopo wa misimu miwili staa wa Colombia, James Rodriguez aliyetokea Real Madrid. Wengine ni Corentin Tolisso aliyetokea Lyon na Kingsley Coman aliyetokea Juventus. Hapana shaka kwa Ujerumani, Bayern ndio timu ambayo kwa mbali sana inaongoza kwa kulipa mishahara mikubwa.

Arsenal (Pauni 210 milioni)

(Wanaoongoza: Mesut Ozil, Alexis Sanchez, £150,000 kwa wiki)

Mwishoni mwa Septemba, Arsenal walitangaza ongezeko la mishahara yao ambapo bili ilifikia pauni 199 milioni. Hata hivyo, dau hili linabakia kuwa dogo licha ya kutua kwa Alexandre Lacazette na inaonyesha jinsi gani ambavyo kocha wao, Arsene Wenger anaiongoza klabu hiyo kwa faida zaidi.

Bado mishahara yao sio mikubwa kulinganisha na wapinzani wao katika Ligi Kuu ya England. Klabu ambayo inaonewa na Arsenal ni Liverpool tu, miongoni mwa vigogo wanaopambana kwenye Top Six.

Liverpool (Pauni £210 milioni)

(Anayeongoza: Philippe Coutinho, £200,000 kwa wiki)

Inaonyesha jinsi gani mambo yanavyobadlika kwa haraka zaidi katika soka. Msimu mmoja tu uliopita Liverpool walikuwa wanalipa mishahara mikubwa kuliko Manchester City. Leo Liverpool wapo chini kwa mbali kulinganisha na Man City.

Kama wakiibiwa Philippe Coutinho na Barcelona bila ya kununua wachezaji wenye majina makubwa basi Liverpool itakwenda chini zaidi.

Juventus (Pauni 150 milioni)

(Anayeongoza: Gonzalo Higuain, £130,000 kwa wiki)

Hii inakuonyesha jinsi gani ambayo soka la Italia limerudi chini kwa kiasi kikubwa. Kama zingekuwa zama za akina Ronaldo de Lima si ajabu Italia ingekuwa inaongoza lakini sasa klabu kubwa zaidi nchini Italia kwa sasa, Juventus inashika nafasi ya 10 kwa kulipwa mishahara mikubwa Ulaya.

Kwa sasa wanalipa kiasi cha pauni 150 milioni kwa mwaka na wanabakia kuwa klabu pekee ya italia katika kumi bora. Kwa pale Italia wanafuatiwa na AC Milan ambayo inalipa kiasi cha pauni 107 milioni tu kwa mwaka. Hata hivyo, kwa sasa Juventus ndio vinara wakibeba mataji ya Italia mfululizo na kuzipiga bao Inter na AC ambazo zilikuwa moto kwelikweli.