PESA WANAYOLIPWA KWA KUVAA TU VIATU, NI NOMA

HIVI vuta fikira viatu unavaa wewe na pesa unalipwa wewe. Hayo ndiyo maisha ya wanasoka yalivyo kutokana na vile viatu wanavyovaa wanapocheza mchezo huo.

Katika soka la kulipwa, karibu wanasoka wote wanalipwa mishahara mikubwa na bado wa madili ya maana kutokana na viatu wanavyovaa wakati wa mechi, lakini kuna mastaa hawa saba ndiyo wenye madili ya pesa nyingi kutokana na viatu wanavyotinga kwenye mechi.

7.Marco Verratti

(Nike, Pauni 2.7 milioni)

Utashangaa kuona kwenye orodha hii halipo jina la Lionel Messi, lakini ukweli ndio huo, mkwanja anaovuta staa huyo kupitia dili lake la viatu anavyovaa ni mdogo kuliko anaokamatia kiungo wa Kitaliano, anayekipiga kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain, Marco Verratti.

Huko PSG, Verratti ni staa mkubwa japo siku za karibuni kumekuwa na ripoti staa huyo anaweza kuachana na maisha hayo ya Paris na kutimkia kwingineko. Nike inampa Verratti mkwanja wa Pauni 2.7 milioni kwa mwaka kutokana na kuvaa viatu vyao, pesa ambayo ni kubwa kuliko wanayolipa kutokana na miguu ya Messi kuvaa viatu vya kampuni hiyo.

6. Paul Pogba

(Adidas, Pauni 3.1 milioni)

Paul Pogba ni nembo inayotembea, hivyo ni kitu kisichoshangaza kuona naye yumo kwenye orodha ya mastaa wa soka wanaovuna pesa nyingi kutokana na dili za viatu vyao wanavyovaa kwenye mechi za mchezo huo.

Huko Ligi Kuu England, Pogba ndiye mchezaji ghali zaidi kutokana na uhamisho wake kuigharimu Manchester United Pauni 89 milioni, ilipomnasa kutoka Juventus. Pogba ni shabiki mkubwa sana wa adidas, amekuwa akivaa viatu vya kampuni hiyo hata kama anapokuwa kwenye mambo mengine ya nje ya uwanja.

Kwa kuvaa viatu vya kampuni hiyo kwenye mechi, Pogba analipwa Pauni 3.1 milioni kwa mwaka na hivyo kuwa miongoni mwa mastaa wa soka wanaovunja mkwanja mrefu kupitia dili la viatu.

5.Mesut Ozil

(Adidas, Pauni 3.7 milioni)

Kiungo Mjerumani, Mesut Ozil amesaini dili jipya la kuendelea kuichezea Arsenal na sasa anavuna mshahara mrefu si mchezo, kuanzia Pauni 300,000 kwa wiki.

Mashabiki wa Arsenal wanamatumaini makubwa kutoka kwa fundi huyo wa mpira atawafanya kuwa bora zaidi na kufanya mambo makubwa ndani ya uwanja kwa miaka mingine kadhaa.

Huduma bora ndani ya uwanja, imewafanya Adidas pia kusaini naye dili tamu ambalo linamfanya Ozil avune mkwanja wa kutosha kutoka kwao kila anapovaa viatu hivyo.

Zile asisti zake ndizo zinazoifanya Adidas kumlipa Ozil Pauni 3.7 milioni kwa mwaka kutokana na kuvaa viatu vyao.

4. Cesc Fabregas

(Puma, Pauni 4 milioni)

Kiungo fundi wa mpira kutoka Hispania, Cesc Fabregas amekuwa kwenye mikono ya Puma tangu zama hizo alipokuwa mchezaji wa Arsenal.

Alikwenda Barcelona akiwa na wadhamini hao hao wanaompa viatu vyake anavyowatesa wapinzani ndani ya uwanja na sasa yupo kwenye kikosi cha Chelsea kwenye Ligi Kuu England. Puma wamenogewa na kuendelea kuitumia huduma ya kiungo huyo kutokana na kumpa viatu ambavyo vinampa urahisi wa kupiga zile pasi zake za mwisho ndani ya uwanja.

Alipotua Stamford Bridge, Puma iliboresha dili lake na hivyo kumlipa kiungo huyo Pauni 4 milioni kwa mwaka kutokana na kutupia kiatu cha Puma anapoingia uwanjani kukipiga.

3.Gareth Bale

(Adidas, Pauni 4.1 milioni)

Staa wa Real Madrid, Gareth Bale, ndiye mchezaji anayeshika namba moja kwa wanaovuna pesa nyingi kwa kuvaa viatu vya Adidas.

Bale wakati anatoka Tottenham Hotspur kwenda Real Madrid dili lake la uhamisho lilivunja rekodi ya dunia, Pauni 85 milioni na kufanikiwa kusaini dili matata la viatu anavyotumia kucheza soka lake.

Licha ya kwamba amekuwa si mchezaji wa kutumainiwa sana huko Santiago Bernabeu, huku akitajwa kwenye ile orodha ya wale watakaofunguliwa mlango wa kutokea dirisha lijalo la usajili, bado ni mchezaji muhimu kwa Adidas na ndiyo maana inamlipa Pauni 4.1 milioni kwa mwaka kuvaa viatu vyao.

2. Mario Balotelli

(Puma, Pauni 5.1 milioni)

Usishangae, huo ndio ukweli. Straika Mtaliano, Mario Balotelli ndiye mchezaji anayeshika namba mbili kuwa na dili la viatu lenye thamani kubwa zaidi kwenye soka. Ukorofi wake wa uwanjani, kamwe haukumweka mbali na dili za maana kama hizo.

Fowadi huyo anayekipiga kwenye kikosi cha Nice, anavaa kiatu cha Puma, ambacho kinamfanya awe mchezaji namba mbili anayelipwa pesa nyingi kwa kutumia viatu hivyo.

Balotelli, aliyewahi kuzichezea Manchester City na Liverpool Ligi Kuu England, analipwa Pauni 5.1 milioni kwa mwaka kwa kuvaa viatu vya Puma.

1.Cristiano Ronaldo

(Nike, Pauni 6.2 milioni

Katika kuelekea Kombe la Dunia 2018 litakalofanyika huko Russia, Nice imemtengenezea supastaa Cristiano Ronaldo viatu vipya kabisa ambavyo atavaa katika fainali hizo akiwa na chama lake la Ureno.

Mkataba wa Nike na Ronaldo ni wa muda mrefu sana na ndiyo maana kuona haishangazi kwa staa huyo kuvalishwa viatu vya kijanja, huku akivuna pesa ndefu. Kwa dili la viatu, Ronaldo ndiye mwenye mkataba wenye pesa nyingi zaidi kutokana na viatu hivyo vya Nike anavyofaa kwenye mechi kumwingizia mzigo wa Pauni 6.2 milioni kwa mwaka.