PACHA YA NGOMA..

Muktasari:

Kutokana na uwepo wa mastaa hao, kukosekana kwa Obrey Chirwa na Papy Kabamba Tshishimbi, hakuwezi kuwa na athari kubwa kwa Yanga.

HARAKATI za kusaka ushindi zimeanza kwa mabosi wa Yanga baada ya kung’olewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa Kombe la Shirikisho. Baada ya droo ya Caf kufanyika na kupangwa kuanza na Welayta Dicha ya Ethiopia, jana mabosi wa timu hiyo wameanza vikao kuhakikisha wanashinda huku uwepo wa straika matata Ibrahim Ajibu na kurejea kwa Donald Ngoma, hakujawapa shaka Yanga.

Kutokana na uwepo wa mastaa hao, kukosekana kwa Obrey Chirwa na Papy Kabamba Tshishimbi, hakuwezi kuwa na athari kubwa kwa Yanga.

Hata hivyo, kelele huko mtaani zimekuwa zikivuma kuwa wapinzani wa Yanga ni dhaifu huku upande wa pili, wakiwaonya wenzao wakiwataka kwenda kujifunza kwa Zamalek.

Lakini, takwimu haziongopi kabisa kwani, wapinzani hao wa Yanga wanaonekana kuwa ni wepesi na wanapiga tu uwanjani. Wakati Yanga ikishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 21, Welayta Dicha inayoshiriki Ligi Kuu nchini kwao ipo nafasi ya nane ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 15.

Pia, Dicha wanaonekana kuwa na ukuta dhaifu, kwani wamefunga mabao 14 na kuruhusu wavu wake kutikiswa kwa idadi hiyo hiyo ya mabao tofauti na Yanga, ambao wamekuwa imara kwelikweli licha ya kupitia kipindi kigumu kwa sasa.

Katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho, Wahabeshi hao walipokutana na Zimamoto ya Zanzibar walilazimisha sare ya bao 1-1 ugenini kisha kuibuka na ushindi wa bao 1-0 wakiwa kwao. Walipovuka hatua hiyo walikutana na Zamalek ya Misri na kushinda mabao 2-1 nchini Ethiopia, lakini waliposafiri ugenini wakipanda ndege moja na Simba wakati wakiwafuata Al Masry, walipokea kipigo cha mabao 2-1 na kusonga mbele kwa ushindi wa matuta.

Katika ligi ya kwao wameshinda mechi tano pekee wakipoteza sita na kutoa sare nne huku Yanga wakipoteza mechi moja pekee wakipata ushindi mara 13 na sare zikiwa saba.

Hata hivyo, kabla Yanga hawajakutana na Wahabeshi hao kikosi hicho cha Kocha, George Lwandamina kitajiweka sawa kutatua changamoto mbalimbali kabla ya kushuka Uwanja wa Taifa, April 7.

Uwanja wa

nyumbani

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa ameliambia Mwanaspoti wamefanya tathimini na kubaini katika misimu miwili mfululizo ya michuano ya kimataifa, wametupwa nje ya mashindano kutokana na kushindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani.

Alisema walipokutana na Zanaco msimu uliopita walishindwa kulinda ushindi wa bao 1-0 na kujikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1 kisha kuondolewa kwa bao la ugenini na hilo limetokea tena msimu huu dhidi ya Township Rollers ya Botswana, kwa kupoteza nyumbani kwa mabao 2-1 na kupata suluhu ugenini.

“Tunajipanga ili kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani, kama tukiweza mipango vizuri nyumbani basi tunaweza kusonga mbele kwani, ugenini tumekuwa na matokeo mazuri,” alisema Mkwasa.

Tshishimbi, Chirwa

Inafahamika Yanga itawakosa mastaa wake, Said Makapu, Pappy Tshishimbi na mshambuliaji Obrey Chirwa wanaozuiwa kikanuni baada ya kufikisha kadi mbili za njano. Hata hivyo, kabla ya kuivaa Dicha, Lwandamina amekuna kichwa kusaka mbadala wa nyota hao.

Katika maandalizi ya mchezo huo, Lwandamina amesema Jumatatu ataanza kazi ya kusaka wachezaji watakaopewa jukumu la kuziba nafasi hizo.

“Tunajua tunatakiwa kuziba nafasi hizo, haitakuwa kazi rahisi, ni lazima tujipange na kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya mchezo huo. Ukiangalia hawa wachezaji ni muhimu na walikuwa na majukumu tofauti uwanjani,” alisema Lwandamina.

Yanga washtuka

Mastaa wa Yanga waliahidiwa donge nono kama wangeitupa nje Rollers, lakini mambo yakawa magumu. Lakini, kwa sasa wameshtuka mapema na wameapa wapinzani wao wakikanyaga tu Taifa ni lazima waumie.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, beki Haji Mwinyi na Hassan Kessy, wamesema wana imani watafika hatua ya makundi tena kwa kupitia ushindi wa nyumbani.

“Tumetolewa kirahisi sana na Township Rollers na hilo limetupa fundisho kubwa na sasa hatutafanya makosa tena kwa kushindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

“Ili tufike mbali, nidhamu ya mchezo inatakiwa na hii ni fursa nyingine ya kurekebisha makosa yetu uwanjani. Lazima wapinzani wafe hapa nyumbani na tukienda kwao tunakaza kama kawaida,” alisema Kessy.

Kwa upande wao, Emmanuel Martin na Yohana Mkomola, walisema mabao mengi ya nyumbani ndio yatakayowaweka salama.

“Tunatakiwa kujipanga na kufunga mabao mengi nyumbani ili ugenini twende kushambulia kwa kushtukiza, naamini tutapiga hatua,” alisema Martin.

“Hata kama wapinzani hatuwajui, muhimu ni kushinda nyumbani na kulinda mabao ugenini,” alisema Mkomola.