Oscar Joshua wala hana kinyongo

Muktasari:

  • Beki huyo mwenye mwili jumba, alisema anaondoka Yanga huku akiendelea kuikumbuka kwa mengi iliyomfanyia na kumsaidia kupanua upeo wake katika soka la kitaifa na kimataifa na sasa anajipanga kuibuka kwingine.

OSCAR Joshua ni miongoni mwa wachezaji wa muda mrefu waliokuwa ndani ya Yanga lakini ameachwa katika kikosi cha msimu ujao. Hata hivyo mwenyewe amesema wala hana kinyongo kwa sababu maisha ndivyo yalivyo.

Beki huyo mwenye mwili jumba, alisema anaondoka Yanga huku akiendelea kuikumbuka kwa mengi iliyomfanyia na kumsaidia kupanua upeo wake katika soka la kitaifa na kimataifa na sasa anajipanga kuibuka kwingine.

“Yanga, ina watu tofauti na wenye kazi tofauti, nilikuwa makini kutumia nafasi hizo ili kujifunza mengi yenye faida kwa maisha yangu, sitaacha kuishukuru na kuachwa kwangu hakuwezi kujenga uhasama nao,” alisema Oscar ‘OJ’.

“Sitaisahau Yanga, imefanya niwe nilivyo leo, siwezi kutaja vitu nilivyovipata kwani ni vingi ila itabaki akilini na kuipa heshima kama moja ya alama ya mafanikio yangi kimaisha.

Kuhusu usajili mpya Jangwani na hasa kwa nyota wa kigeni, beki huyo wa kushoto alisema ni lazima wafanye mambo makubwa kujitofautisha akimtolea mfano Mbuyu Twite aliyeondoka Jangwani akiwa na heshima kubwa kwa kazi aliyofanya.

“Wajue kuwa kusajiliwa kwao pale Yanga maana yake wanatakiwa kujituma,” alisema.