Ongala awapiga chini wachezaji 16, Majimaji kusajili 11 wapya

Muktasari:

  • Ongala amechukua uamuzi huo kwa sababu wachezaji hao walishindwa kuonyesha kiwango cha kuridhisha pamoja na utovu wa nidhamu.

Baada ya kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu huu kocha Majimaji, Kally Ongala Majimaji ameamua kuachana na wachezaji 16 ili kusuka upya kikosi kwa ajili ya msimu ujao.

Ongala amechukua uamuzi huo kwa sababu wachezaji hao walishindwa kuonyesha kiwango cha kuridhisha pamoja na utovu wa nidhamu.

Mwenyekiti wa Majimaji, Humphrey  Milanzi amesema wanaachana na wachezaji hao kutokana ripoti ya kocha wao.

Aliwataja baadhi ya wachezaji walioachwa ni George Mpole , Peter Joseph, Yussuf  Mfanyaje , Ibrahim Tende , Agathon Antony, Sagath Mohamed.

Alisema wachezaji hao tayari wamekabidhiwa mikoba yao ili watafute timu zingine za kuzitumikia kwa msimu ujao.

 Milanzi alisema hadi sasa Majimaji imebakiwa na wachezaji 13 pekee huku wakitaka kusajili wachezaji 11 wapya na wengine kutoka timu ya vijana.

 ‘’Bado hatujaingia nao mikataba kwa hiyo kuwataja inakuwa ni vigumu ila tunaendelea na mazungumzo nao na hatimaye wakikubali kusaini ndipo kila kitu kitawekwa wazi.

Hata hivyo taarifa zinadi kuwa ripoti hiyo ya Ongala iliwataka wachezaji Yusuph Ndikumana kutoka Mbao, Kigi Makasi wa Ndanda FC  pamoja na  Jacob Masawe wa Stand United.