Omog akitua tu, Mzambia anasaini

WAKATI aliyekuwa Nahodha wa Simba, Method Mwanjali, amekubali kiroho safi kumpisha Mghana, Asante Kwasi kuchukua nafasi yake kikosini, straika kutoka Zambia, Jonas Sekuhawa anamsubiri Kocha Jospeh Omog atue tu Dar ili asaini.

Omog aliyekuwa kwao Cameroon kwa mapumziko ya wiki mbili anatarajia kutua leo Alhamisi tayari kuendelea na kibarua chake cha kuiandaa Simba kwa mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda na ile ya Kombe la FA.

Simba imepangwa kuanza na Green Worriors katika mechi ya 64 Bora ya michuano hiyo maarufu kama Azam Sports Federation Cup na ikimaliza mechi hiyo hiyo itasafiri hadi Mtwara kucheza mechi ya ligi na Ndanda.

Timu hiyo imetangaza kuachana na aliyekuwa nahodha wake, Mzimbabwe Mwanjali ambaye amekubali kiroho safi kutemwa kwa makubaliano na viongozi wa timu hiyo, lakini wanamsubiri Omog wamsainishe Mzambia.

Kocha Omog, anatarajiwa kutua leo na moja kwa moja baada ya kuwasili anatarajiwa kutoa maamuzi juu ya Sekuhawa ambaye amelivutia benchi la ufundi la Simba lililokuwa chini ya Kocha Msaidizi Mrundi Masudi Djuma.

Ipo hivi. Kamati ya Usajili ya Simba tayari inayo majina mawili mezani ya wachezaji wa kigeni ambao ni Asante Kwasi na ambaye

Mwanaspoti linafahamu Jumatatu alikuwa asaini, lakini viongozi wa Lipuli wakataka kwanza wamaliziwe makubaliano waliyoingia na Simba ili beki huyo avae uzi wa Msimbazi.

Jina jingine ni la Sekuhawa ambaye anasubiri kauli ya Omog kama asaini au la ikizingatiwa zimesalia kama saa 24 tu kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, huku kila kitu kikiwa kipo sawa kwa viongozi na wasaidizi wa Omog.

“Suala la Kwasi kila kitu kilienda sawa na alikuwa aje kusaini mkataba Jumatatu jioni, lakini mabosi wa Lipuli walizuia kwanza kwani kuna mambo walikuwa wanataka tuwamalize kwani wana mkataba naye, “ alisema mmoja wa viongozi wa Simba.

Naye Meneja wa Simba, Richard Robert ‘Mwana’ alisema kamati yao ya usajili inapambana na muda uliosalia kukamilisha maelekezo ya ripoti ya kocha ya kusajiliwa straika na tufuru inaelekea kumuangukia Sekuhawa.

MAPINDUZI FRESHI

Kocha Msaidizi, Masudi Djuma, amesema wapo tayari kulianzisha kwenye Kombe la Mapinduzi walikopangwa Kundi A lenye pia timu za Azam, Jamhuri SC, Mwenge SC na URA ya Uganda.

“Hatuna presha kwani tumejiandaa vilivyo,” alisema.