Olunga aingia anga za Messi leo

Muktasari:

Mshambuliaji huyo amekuwa Mkenya wa kwanza kufunga mabao matatu katika mechi moja ya La Liga

BARCELON, HISPANIA. Macho ya mashabiki wa soka wa nchi za Afrika Mashariki hii leo Jumamosi yatakuwa huko kwenye Uwanja wa Nou Camp kuona kama mshambuliaji wa Kenya, Michael Olunga ataweza kuwapiga bao Barcelona wakati kikosi chake cha Girona kitakapokwenda kucheza na timu hiyo kwenye mchezo wa La Liga.

Olunga wiki za karibuni tu aliandika rekodi ya kupiga hat-trick katika ligi hiyo, hivyo hii leo anatazamiwa kuwaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa Barcelona wakiongozwa na Gerard Pique.

Hata hivyo, hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Girona kwenda kucheza Nou Camp katika mechi ya La Liga, huku wakienda kukutana na Lionel Messi, ambaye ndiye iliyokuwa timu ya kwanza kuifunga wakati Muargentina huyo alipokuwa Barcelona B na kukutana nao kwenye Segunda B, Septemba 5, 2004.

Miaka 15 sasa inaelekea, Girona anakwenda kukutana na Messi kwenye La Liga na kuwa timu pekee ambao ndiyo hasa hawajafungwa na staa huyo inapokuja michuano ya La Liga.

Ukiweka kando mechi hiyo ya majirani huko Catalan, mechi nyingine za La Liga zitakazopigwa wikiendi hii, Real Madrid wao watakuwa Bernabeu kuwakaribisha Deportivo Alaves, wakati Celta de Vigo watawakaribisha Eibar na Leganes watakipiga na Las Palmas.

Kesho Jumapili, Villarreal watakuwa wenyeji wa Getafe, wakati Athletic Bilbao watacheza na Malaga, Valencia na Real Sociedad na Sevilla wataonyeshana ubabe  na wababe wenzao, Atletico Madrid.