Okwi akizingua tu imekula kwake

Tuesday July 11 2017

 

By OLIPA ASSA

KIUNGO wa zamani wa Simba, Mohammed Banka amemtaka mshambuliaji mpya wa Simba, Emmanuel Okwi kujitahidi kulinda heshima yake aliyoiacha nchini miaka michache iliyopita wakati anatimkia Denmark.

Banka ambaye aliwahi pia kucheza Yanga na Moro United, alisema kwa namna ambavyo Okwi ametukuka Simba, basi atapaswa kufanya utafiti kujua kiasi gani anapewa kipaumbele ili asije akajikuta heshima yake inayeyuka.

“Hili picha linajirudia kama lilivyokuwa kwa Mavugo (Laudit). Mashabiki walimgoja kwa kitambo kirefu lakini baadaye hakufikia mafanikio ambayo yalitarajiwa na wengi. Ndivyo ilivyo kwa Okwi, Simba ilifanya vibaya lakini viongozi waliposema Okwi anakuja mashabiki walitulia,” alisema.

Licha ya kukiri kuwa Okwi ni mchezaji mzuri, Banka alimtahadharisha wasiwasi ndiyo akili na yeye ni mkongwe na anapaswa kuwa mfano wakati wote.

“Shujaa ni yule anayelinda heshima yake hadi anapostafu na siyo kuishia njiani, ujio wake unafanya watu waanze kutamba mitaani kabla ya kuanza kwa ligi yenyewe,” alisema Banka.