Okwi akitoa mbio za ufungaji bora

Muktasari:

Mshambuliaji huyo msimu uliopita aliweka rekodi yake ya kuwa mfungaji bora kwa Ligi Kuu bara kwa mara ya kwanza

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amesema wala hana presha ya kufunga mabao 20 kama alivyofanya msimu uliopita bali anachoangalia ni ushindi wa timu kwanza.

Okwi aliibuka mfungaji bora msimu uliopita akipachika wavuni mabao 20, lakini mpaka sasa Ligi Kuu Bara ikiingia raundi ya nne hajafunga bao lolote.

Mshambuliaji huyo raia wa Uganda hajaichezea Simba mechi yoyote tangu Ligi Kuu ianze msimu huu kutokana na kuwa majeruhi alianza katika katika mchezo wa leo dhidi ya Ndanda, lakini alishindwa kumaliza baada ya kuumia.

Okwi alisema yoyote atakayefunga ndani ya kikosi hicho kwake sawa tu ili mradi timu ipate ushindi.

"Muhimu hapa ni timu kupata ushindi. Timu kwanza mtu baaade. hivyo nifunge mimi au afunge mwingine yote sawa ili mradi tupate pointi tatu.

"Sina presha ya ufungaji bora msimu huu kwani hata kama msimu uliopita nilifunga mabao 20 na nikaibuka mfungaji bora hainifanyi niwaze zaidi kuchukua tuzo hiyo tena kwani ninachoangali ni kuipa mafanikio timu kwanza "alisema Okwi.

Ujio wa Mnyarwanda Meddy Kagere mwenye mabao matatu kwenye ligi umeonekana kutikisa ufalme wa mchezaji huyo ndani ya Simba ingwa bado kuna ubishani miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo wakihoji nani mkali zaidi ya mwenzake.