Okwi aitaka Yanga mapema

MFUNGAJI Bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Mganda Emmanuel Okwi aliyefunga mabao 20 amesema wapo tayari na wameiva kupambana na timu yoyote ambayo itakuwa mbele yao msimu huu.

Mwanaspoti iliweka kambi katika uwanja wa ndege Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo ilishuhudia nyota wote wa Simba wakitua na wakitawanyika majumbani kwao ambapo walipewa mapumziko ya siku mbili, huku wakifanya mazoezi katika uwanja wa Uhuru wakitokea majumbani mwao.

Okwi alisema kwanza anawapongeza viongozi wa Simba kwani amecheza misimu mingi katika timu hiyo lakini safari hii wameonekana kujipanga mno kwani tangu amekuwa hapo kwa miaka yote hawajawahi kuweka kambi nje ya Tanzania.

Alisema hii ni ishara tosha kuna kitu kikubwa wachezaji tunadaiwa mbele yetu kwani nadhani ni maandalizi bora ambayo tumeyafanya kulijko timu yoyote hapa nchini.

“Maandalizi haya tuliyofanya ni ya hali ya juu na si kushindana na Yanga bali ni timu yoyote ile ambayo itakuwa mbele yetu kutoka ndani ya nchi hata zile ambazo tutakutana nazo katika mechi za Kimataifa,” alisema.

“Kama wachezaji tuliokuwa katika kambi hii tunatambua tunadeni kubwa la kulilipa kwa benchi la ufundi, viongozi, wanachama na wapenzi wa Simba kwa kuwapa matokeo ya ushindi katika kila mechi ingawa kuna ambazo tunaweza kupoteza pia.

“Kwangu ninadhani nilipata maandalizi na mazoezi ya kutosha ambayo mengine nitaendelea kuyapata lakini natambua kubwa ninadeni na kulipa au kuendelea kuwa katika kiwango bora kama au zaidi ya msimu uliopita mbapo nilikuwa mfungaji bora,” alisema Okwi.

“Natambua nitakuwa na msimu mgumu kwani kila beki ambaye nitakutana naye atataka kunizuia lakini nimejipanga na ninamuomba Mungu anisaidie niweze kushindana nalo hilo na kufunga kama msimu ulioisha na hata Simba pia tunaweza kukutana na ugumu katika mechi za ligi kwani siku zote bingwa mtetezi anakamiwa,” aliongeza Okwi.

Okwi aliondoka na gari aina ya Brevis ambayo ilikuwa ikiendeshwa na mratibu wa Simba, Abbas Selemani akiwa sambamba na Meddie Kagere, Pascal Wawa na kiungo mpya Mzambia, Cletus Chama.

“Maandalizi yalikuwa mazuri na yakutosha kabisa kulingana na ambacho tulikuwa tunahitaji nadhani kazi iliyobaki ni kwenda kutumia hiki ambacho tumekipata Uturuki katika kila mechi ya kimashindano,” alisema.

Mbali na ligi, Simba inajiandaa kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia Desemba mwaka huu.